Habari
Ofisi ya Makamu wa Rais kuratibu utekelyezaji wa Dira ya 2050
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni amesema katika mwaka wa fedha 2026/27 Ofisi imepanga mambo mbalimbali katika suala la Uhifadhi na Utunzaji wa Mazingira ikiwa pamoja na Kuratibu utekelezaji wa Dira ya 2050.
Ameyasema hayo Machi 24,2026 wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mpango na bajeti kwa mwaka wa fedha 2025/26 na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2026/27 kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira.
Mhe. Masauni amesema Ofisi itatekeleza sera ya Taifa ya Mazingira 2021 na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, Sura 191 na Kusimamia Utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Taifa wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (2022-2032).
“Kuimarisha uratibu na utekelezaji wa masuala ya hifadhi na usimamizi wa mazingira katika Wizara za Kisekta, taasisi, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na wadau mbalimbali wa mazingira” amesema Mhe. Masauni.
Ameongeza kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais, imepanga kutoa Elimu kwa Umma kuhusu Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi eneo ambalo , litaangaliwa kwa upana zaidi.
Ameongeza kuwa Ofisi itaendelea kuratibu utekelezaji wa Mikataba ya Kikanda na Kimataifa inayohusu hifadhi na usimamizi wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi ambayo Tanzania ni nchi mwanachama pamoja na masuala mengineyo yanayohusu Uhifadhi na Utunzaji wa Mazingira.



