Naibu Waziri Khamis akemea uvamizi hifadhi ya Mlima Kilimanjaro

Jul, 22 2024

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis amewataka wananchi kuacha kuvamia vyanzo vya maji katika maeneo yanayozunguka hifadhi ya Mlima Kilimanjaro.

Amesema hayo wakati akizindua na kushiriki Kampeni ya ‘Save Mount Kilimanjaro’ (Okoa Mlima Kilimanjaro) yenye lengo la kuchangia upandaji wa miti zaidi ya bilioni 1 kwa mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara na Tanga.

Mhe. Khamis amesema kumekuwa na baadhi ya wananchi wanafanya shughuli za kibinadamu zikiwemo kilimo, uchimbaji wa madini na uchomaji moto misitu hivyo kusababisha uharibifu wa mazingira.

Kutokana na hali hiyo, ametoa wito kwa wadau na jamii kwa ujumla kupanda miti kwenye eneo la mlima huo ili kusaidia kuokoa barafu isiyeyuke kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi zinazoikabili dunia.

Akizungumza wakati wa kampeni hiyo iliyoambatana na matembezi ya hisani ya kilomita 6, 10 na 16, Mhe. Khamis amesema Mlima Kilimanjaro ni moja ya tunu za Taifa, hivyo upandaji wa miti hii utasaidia kuokoa barafu yake ambayo ni kivutio kikubwa kwa watalii kuja kuupanda na kuishuhudia barafu hiyo”

“Niwapongeze Taasisi ya Nessa Foundation kuja na Kampeni hii itakayosaidia kuimarisha ikolojia ya hifadhi yetu ya Kilimanjaro, pia upandaji wa miti utaongeza kiasi cha mvua kwa mikoa hii ya kaskazini na hivyo kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi,” alisema.


Settings