Habari
Dkt Muyungi: Biashara ya kaboni kuingiza bilioni 2 kila mwaka
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Richard Muyungi amesema biashara ya kaboni ni moja ya malengo ya Serikali katika kukuza uchumi ifikapo mwaka 2050 na kwamba kuna uwezekano wa kuingiza shilingi bilioni 2 kila mwaka.
Ametoa kauli hiyo wakati akiwa katika mashamba ya mwekezaji wa shughuli za kilimo wilayani Kyerwa mkoani Kagera Leonard Kachebonaho ambaye kampuni hiyo inajishughilisha na biashara ya kaboni.
Inaelezwa kuwa hadi sasa wakulima zaidi ya 100,000 wamesajiliwa na wameanza kunufaika na biashara hiyo.
Dkt. Muyungi alisema kuwa Serikali ina malengo ya kukuza uchumi wake kupitia vyanzo mbalimbali ikiwemo biashara ya kaboni ambayo ni mpya kwa ulimwenguni na yenye faida kubwa kwa mwananchi mmoja mmoja hasa mkulima pamoja na taifa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Bw. Leonard Kachebonao alisema kuwa shamba hilo linatumika kama shamba darasa kwa wakulima kujifunza namna ya kulima kilimo mseto ambacho licha ya mkulima kupata fedha kupitia mazao anayovuna atapata fedha kupitia uvunaji wa hewa ya kaboni.
Katika hatua nyingine, Dkt. Muyungi aliwapongeza wadau wa mazingira kwa uzalendo na uwekezaji wao katika afua za mazingira na kutatua changamoto za jamii.
Alitoa pongezi hizo wakati alipotembelea Shule binafsi ya Hosiana English Medium Primary School iliyopo wilayani Karagwe Mkoa wa Kagera.
Shule hiyo inatumia umeme jua (solar) kupika chakula cha wanafunzi zaidi ya 200 hatua ambayo inaonesha kutekeleza maelekezo ya Serikali kwa taasisi zinazolisha watu zaidi ya 100 kutumia nishati safi kupikia.
Matumizi ya nishati safi ya kupikia ni njia mojawapo ya kupunguza vitendo vya ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na kuchoma mkaa, ambavyo vinachangia uharibifu wa mazingira.
Hivyo, Dkt. Muyungi aliuhimiza uongozi wa Mkoa wa Kagera kuongeza juhudi kwa za kuhamasisha taasisi zinazolisha watu zaidi ya 100 kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Pia, Katibu Mkuu huyo alitumia ziara hiyo kutembelea kiwanda cha kuchakata kahawa cha KADERES katika Kijiji cha Kitwe wilayani Kyerwa kwa ajili ya kujionea shughuli mbalimbali.



