Naibu Waziri Chande azitaka Halmashauri kuzibana kumbi za starehe zinazopiga kelele maeneo ya makazi

Oct, 17 2021

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Hamad Hassan Chande amezitaka halmashauri nchini kuhakikisha zinadhibiti nyumba za starehe zinazopiga muziki wenye kelele katika maeneo ya makazi ya watu.

Alisema kuna baadhi ya maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya makazi lakini ghafla maeneo hayo yanatumiwa kwa shughuli zisizopangwa kama vile kumbi za starehe na kuleta usumbufu wa kelele kwa wananchi.

“Katika halmashauri kuna maeneo yaliyopangwa kwa ajili ya makazi na shughuli nyingine lakini ghafla maeneo hayo yanabadilika na kuwa kumbi za starehe zinazopiga muziki unaoleta kelele na kukera watu, huu muhali tuuondoe,” alisema Chande.

Aliongeza kuwa halmashauri nchini zinatakiwa kusimamia mipango yake kwa kuhakikisha shughuli zinazofanyika katika maeneo yake ni zile zilizopangwa kwa kuwa mara kadhaa kumekuwa na malalamiko kuhusu muingiliano wa nyumba za makazi na kumbi za starehe.

Naibu Waziri Chande ambaye alikuwa akizungumza mwishoni mwa wiki wakati wa kikao kati ya Kamati ya Mawaziri 8 wa Wizara za Kisekta na viongozi wa mkoa wa Geita alisema nyumba za starehe zinazopiga kelele za muziki kwenye maeneo ya makazi zimekuwa zikileta athari ikiwemo kwa wagonjwa wa moyo na kuzua malalamiko miongoni mwa wananchi ambapo alizitaka halmashauri zote nchini kutofumbua macho suala hilo.

Alisisitiza kwa kusema kuwa, kama nyumba imepangiwa matumizi ya makazi basi itumike kwa suala hilo na si vinginevyo na kubainisha kuwa, halmashauri zihakikishe zinaandaa na kusimamia mipango ya matumizi bora ya ardhi kwenye maeneo yake.

Akigeukia suala la usimamizi wa mazingira nchini Chande alisema, mazingira ndiyo maisha na uhai wa binadamu na viumbe vingine hivyo wananchi wanatakiwa kuhakikisha wanayatunza ili kuepuka kukosa rasilimali hewa.

“Ukikosa rasilimali hewa uhai na thamani ya ubinadamu imeisha na bila mazingira hakuna mifugo wala maji, mazingira yetu ndiyo maisha na uhai wetu” alisema Chande.

Settings