Makamu wa Rais awataka RUWASA kutoa huduma kwa gharama nafuu

Mar, 20 2023

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amewataka Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kutumia Mitambo ya uchimbaji visima ilionunuliwa na serikali kwa matumizi yaliokusudiwa ikiwemo kutoa huduma kwa wananchi kwa gharama nafuu.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati akikagua magari na mitambo ya uchimbaji visima na mabwawa yaliokabidhiwa kwa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Taarifa ya Utendaji wa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira kwa mwaka 2021/2022 iliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam leo tarehe 20 Machi 2023.

Amekemea mitambo hiyo kutumika kwa matumizi binafsi na kuagiza RUWASA kutambua wanapaswa kutoa huduma zaidi kwa wananchi kuliko kufanya biashara. Aidha Makamu wa Rais ameagiza kufanyika tathmini ya bei zinazotumika na RUWASA kuchimba visima binafsi vya wananchi ili kuhakikisha haziwi juu zaidi ya bei za kampuni binafsi.

Halikadhalika Makamu wa Rais amesema serikali inaendelea kutafuta njia bora na fupi zaidi katika utoaji wa msamaha wa kodi ili kuharakisha utekelezaji wa miradi mbalimbali hapa nchini ikiwemo miradi ya maji.

Akihutubia viongozi wa mamlaka za majisafi na usafi wa mazingira hapa nchini, Makamu wa Rais amewataka kuacha kufanya kazi kwa mazoea ikiwemo kuzoea matatizo ya wateja na hivyo kutotimiza majukumu yao kwa ufanisi. Pia Makamu wa Rais amekemea uwepo watumishi ndani ya Mamlaka za Maji ambao si waajiriwa (vishoka) wanaoendelea kuchafua Wizara na Mamlaka za Maji kwani ndio wanawaunganishia maji Wananchi bila kufuata utaratibu na kusababisha malalamiko mengi na baadhi ya maeneo kukosa huduma hiyo.

Aidha Makamu wa Rais ameziasa Mamlaka za Maji kujiwekea mikakati ya kuboresha huduma, kufanya kazi kwa kujituma, uzalendo, uadilifu na kwa weledi ili Mamlaka hizo ziweze kujiendesha kibiashara kwani huduma za usambazaji wa maji zinazotolewa hivi sasa haziendani na mapato yanayokusanywa.

  • Vilevile Makamu wa Rais amezitaka Mamlaka zote za maji nchini kuhakikisha zinatoa kipaumbele kupeleka maji safi maeneo muhimu ya kutolea huduma za kijamii zikiwemo hospitali, nyumba za ibada, vituo vya afya na shule. Pia amewataka kuongezakasi ya kutoa elimu kwa wananchi na taasisi hizo kuhusu namna ya kuvuna na kuhifadhi maji ya mvua ili kuhakikisha uwepo wa vyanzo endelevu vya maji hususan katika vipindi vya kiangazi.
  • Katika hatua nyingine Makamu wa Rais ameitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) kuongeza nguvu katika kufanya ukaguzi wa ankara za maji zinatolewa kwa wateja wa Mamlaka za Maji zote nchini na zile zitakazobainika kukiuka utaratibu uliowekwa zishughulikiwe kwa mujibu wa taratibu ikiwemo mamlaka zote za maji ambazo zinatoza bei ambazo hazijaidhinishwa na EWURA.
  • Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maji Maryprisca Mahundi amesema matokeo yaliopatikana kwenye sekta ya maji kutokana na udhibiti unaofanywa na EWURA kwa mamlaka za maji ni pamoja na kuhakikisha mamlaka za maji zinaandaa mipango ya biashara ambayo inawawezesha kupata bei za maji. Pia amesema baadhi ya mamlaka za maji zimepunguza utegemezi kwa serikali kwa kulipia gharama za uendeshaji na kutumia mapato ya ndani na mikopo kutekeleza miradi mikubwa ya maji ya kuongeza upatikanaji wa majisafi katika maeneo ya miji wanayoisimamia.
  • Awali Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Dkt. James Andilile amesema lengo la uzinduzi wa taarifa hiyo ni kuibua changamoto zilizopo katika mamlaka za maji na kuwezesha serikali na wadau mbalimbali kuona maeneo ya vipaumbele vya uwekezaji na kuandaa mipango ya kuboresha utoaji huduma za majisafi na usafi wa mazingira.
  • Dkt. Andilile amesema EWURA itaendelea kushirikiana na serikali ili kuhakikisha taifa linakuwa na huduma za maji za kutosha zenye uhakika katika hali endelevu kwa kuhamasisha na kusimamia ufanisi katika utendaji kazi wa mamlaka za maji.
Settings