Makamu wa Rais awataka mabalozi kuweka mbele maslahi ya Nchi

Oct, 01 2021

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango leo Oktoba mosi, 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na waheshimiwa Mabalozi watakaoiwakilisha Tanzania katika nchi za Rwanda, Sweden, Uturuki, Korea Kusini, Uswisi, India na Ethiopia mazungumzo yaliofanyika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma. Mabalozi hao walifika kumuaga kabla ya kuelekea kwenye vituo vyao vipya vya kazi.

Katika mazungumzo hayo Makamu wa Rais amewaasa mabalozi hao kuweka maslahi ya Tanzania mbele wakati wote watakapokuwa wakiiwakilisha nchi katika maeneo yao. Amewaagiza kwenda kufanya kazi kwa bidi na weledi ili kukuza ushirikiano wenye manufaa baina ya Tanzania na maeneo yao ya uwakilishi hasa kwa kuweka mkazo katika Diplomasia ya Kiuchumi.

Amesema ni vema mabalozi hao kwenda kujifunza yale ambayo yanafanyika katika nchi hizo na kuhamisha maarifa hayo kwa lengo la kukuza na kuendeleza uchumi wa Tanzania. Makamu wa Rais ameongeza kwamba nchi wanazokwenda kuiwakilisha Tanzania zina fursa nyingi hivyo ni vema kutafuta fursa hizo kwa ajili ya watanzania . Amewasihi mabalozi kutafuta wawekezaji watakaoweza kuwekeza hapa nchini na hivyo kuimarisha uchumi wa Tanzania.

Makamu wa Rais amesema zipo nchi zilizoendela katika sekta ya utalii hivyo mabalozi hawana budi kujifunza na baadae kuvutia watalii hao kufika Tanzania kwa manufaa ya nchi. Aidha amewaagiza mabalozi hao kuanzisha na kuimarisha ushirikiano wa kibiashara ikiwa pamoja na kutafuta masoko kwa ajili ya bidhaa za Tanzania.

Akizungumza kwa niaba ya mabalozi hao Balozi wa Tanzania nchini Uturuki Mhe. Luteni Jenerali Yakub Mohamed amesema wapokea miongozo yote waliopewa na Makamu wa Rais na hivyo kuahidi kwenda kuiwakilisha vema Tanzania katika vituo vyao.

Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mbarouk Mbarouk pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mhe. Balozi Joseph Sokoine.

Settings