Makampuni ya vinywaji baridi yatakiwa kutumia chupa ambazo ni rafiki kwa mazingira

Oct, 02 2021

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Selemani Jafo, ameyataka makampuni yanayosalisha vinywaji baridi kutumia chupa ambazo ni rafiki kwa mazingira ambazo zinarejelezeka kwa lengo la kutunza mazingira na kupunguza kiwango cha taka za plastiki nchini.

Ameyasema hayo jijini Dar es Salaam leo alipokuwa akizindua chupa mpya ya kinywaji cha Sprite ya kampuni ya coca cola kutoka iliyokuwa ya kijani na kuingiza chupa isiyo na rangi ambayo ni rahisi kurejelezwa. Aidha, aliahidi kutoa ushirikiano kwa makampuni yanayojitokeza kuchukua hatua binafsi za kulinda mazingira kama ilivyofanya Kampuni ya Coca cola.

"Hii ni hatua muhimu sana katika jitihada za kutunza mazingira iliyofanywa na kampuni ya coca cola. Natoa maelekezo kwa makampuni mengine ya vinywaji baridi kuiga mfano wa kampuni ya coca cola kupitia kinywaji cha Sprite kubadili chupa za rangi ili kupunguza taka za chupa za plastiki zenye rangi ambazo zimezagaa mitaani na kuchafua mazingira". Alisema Jafo.

Akirejea maelekezo yake alipotembelea kiwanda cha Coca cola mwezi Septemba 2021, Jafa alisema, "Nilitoa mwaka mmoja kwa wamiliki wa viwanda vya vinywaji baridi kubadili teknolojia na kuachana na chupa za plastiki zenye rangi. Nawapongeza Coca cola kwa kutekeleza maelekezo haya kwa kipindi kifupi na kuonyesha kuwa jambo hili linawezekana. Hivyo viwanda vingine waige mfano huu"

Kwa upande wake Mkurugenzi mkuu wa NEMC Dkt. Samwel Gwamaka aliipongeza kampuni ya coca cola kwa kutekeleza maelekezo ya Serikali kwa hiari na kuzingatia Sheria na Kanuni za kuhifadhi mazingira kwa kubadili chupa ya kinywaji cha Sprite jambo ambalo litapunguza uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na chupa za plastiki kwa kiwango kikubwa.

Awali, akiwasilisha historia ya matumizi ya chupa ya kijani ya Sprite, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Coca cola Tanzania Unguu Sulay, alisema kampuni yake imeamua kubadili cupa ya Sprite ili kuchangia katika utunzaji wa mazingira na kwamba wako tayari kushirikiana na Serikali kuhakikisha taka za plastiki zinadhibitiwa kikamilifu. Aliongeza kuwa katika jitihada hizi wameanzisha kampuni inayojulikana kama PETCO ambayo itajihusisha na kuratibu uzalishaji na urejelezwaji wa taka za plastiki nchini.

"Tumeamua kutekeleza sera ya Dunia bila taka kwa vitendo kupitia mabadiliko haya kwa kuwa chupa mpya ya Sprite inarejelezeka. Tumeamua kuunga mkono jitihada za Serikali kutokomeza taka za plastiki nchini na tumeanzisha kampuni itakayofanya kazi ya ķuratibu masuala ya uzalishaji na urejelezaji wa taka za plastiki hapa Tanzania ili kuhakikisha tunatokomeza taka za plastiki na kuyatunza mazingira".

Settings