Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira yakagua athari za matumizi ya Zebaki kwa wachimbaji wadogo Kahama

Oct, 16 2021

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira wametembelea eneo la wachimbaji wadogo wa dhahabu Mwime katika Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanya leo Oktoba 16, 2021 kukagua athari za matumizi ya Zebaki.

Katika ziara hiyo wajumbe wao waliambatana na Mwenyekiti Mhe. David Kihenzile, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Selemani Jafo na watendaji kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Prof. Esnat Chaggu.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara na wachimbaji wadogo wakati wa ziara hiyo, Mhe. Kihenzile aliwashauri kutazama pia athari za kimazingira wakati wanapofanya shughuli zao ili kuepuka na madhara ya kiafya na kimazingira.

Aidha, aliishauri Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kuendelea kutoa elimu kuhusu athari za kimazingira katika eneo la wachimbaji wadogo pamoja na kupendekeza mbadala wa matumizi ya zebaki kutokana na kuelezwa kuwa na madhara ya kiafya na kimazingira.

“Kwa mfano kwenye eneo la Zebaki bado hatujafahamu kwa kiasi gani athari za Zebaki zimeweza kuathiri wananchi wetu kwa hiyo ni wajibu wako Mheshimiwa Waziri na Serikali kuendelea kutazama na kutafuta pengine mbadala wake kama ni kweli inarithiwa kizazi kimoja kwenda cha pili na cha tatu tuweze kuwakomboa wananchi wetu hawa,” alisema.

Mhe. Kihenzile aliongeza kwa kushauri kuwepo na programu za uhifadhi wa mazingira kwa kuhamaisha upandaji na utunzaji wa miti katika maeneo yote ya wachimbaji wadogo na migodi ili kuepusha kugeuka kuwa jangwa.

Pia wajumbe mbalimbali wa Kamati hiyo pamoja na kupongeza jitihada za Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais na NEMC katika kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo lakini pia walishauri namna bora ya kuhakikisha maji yanaliyotumika kuchenjulia yasitiririke ovyo kwenye makazi ya watu.

Awali akizungumza wakati wa ziara, Waziri Jafo alisema lengo kubwa la ziara hiyo ni kuangalia namna wachimbaji wadogo wanavyozingatia utunzaji wa mazingira katika eneo hilo.

“Kikubwa zaidi katika ziara ya Kamati hii ni kuja kuangalia matumzi ya Zebaki katika kuchenjua na ndio maana iliwapendeza wajumbe kuangalia mchakato mzima toka madini yanavyochimbwa hadi kuchenjuliwa.

“Pia niwaahidi kuwa wataalamu wa mazingira wataendelea kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu katika maeneo mbalimbali nchini huku lakini nanyi pia mtunze mazingira,” alisisitiza Waziri Jafo.

Ziara hiyo iliwahusisha pia Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Bw. Mohammed Khamis Abdulla, Mkurugenzi wa Mazingira, Mwenyekiti wa Bodi ya NEMC, Prof. Esnat Chagu, Mkurugenzi wa NEMC, Dkt. Samwel Gwamaka.

Settings