Habari
Halmashauri ziwe na magari ya taka, madampo
Halmashauri nchini zimetakiwa kuzingatia usimamizi wa taka kwa kutenga bajeti kwa ajili ya kununua magari ya kubebea taka na kujenga madampo yatakayotumika kwa ajili ya ukusanyaji wa taka hizo.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Festo Dugange ametoa rai hiyo wakati wa ziara ya kikazi wilayani Karagwe mkoani Kagera leo Februari 26, 2026 ambapo alizindua mradi wa gari maalumu la kubebea na kusafirisha taka ngumu pamoja na kutembelea Mradi wa Vijana wa Kuchakata Taka za Plastiki.
Amesema kuwa uchafu ukiwemo taka za plastiki ukizagaa bila kukusanywa na kuingia kwenye vyanzo vya maji husababisha maradhi yakiwemo yasiyoambukiza kama vile saratani na shinikizo la damu.
“Ndugu zangu, idadi ya wananchi wanaugua magonjwa kwa sababu ya uchafu wa plastiki na kwenye masoko taka oza au mabaki ya chakula zinapaswa kudhibitiwa na tunaweza kuwa na viwanda vya kuchakata mbolea badala ya kutupa ovyo,” alisema Dkt. Dugange.
Alifafanua kuwa faida za kuwa na madampo ni kuweza kutengeanisha taka za aina mbalimbali kwa mfano taka oza au mabaki ya chakula na taka ngumu ambazo zinaweza kurejelezwa na kutumikia kama rasilimali za kuzalisha bidhaa mbalimbali.
Alisema taka ni mali hivyo, alitumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi kuchangamkia fursa ya taka kwa kuzikusanya na kuziuza kwa viwanda vinavyozalisha bidhaa.
Dkt. Dugange alipongeza hatua ya Halmashauri ya Karagwe ya kuwa na gari maalumu la kukusanya na kusafirisha taka ambalo huku akisisitiza litumike ili kuweka wilaya hiyo katika hali ya usafi.



