Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Makamu wa Rais

Dkt. Muyungi ahimiza utunzaji miradi ya SLR

May, 25 2026

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi, ametoa wito kwa wananchi na wanufaika wa miradi ya maendeleo nchini kuhakikisha wanaitunza na kuiendeleza miradi inayotekelezwa na Serikali pamoja na wadau wa maendeleo, ili iweze kuendelea kutoa manufaa kwa vizazi vya sasa na vijavyo sambamba na kuchochea safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa kati wa juu ifikapo mwaka 2050.

Dkt. Muyungi ametoa kauli hiyo leo Mei 25, 2026 wakati wa ziara yake katika vijiji vya Matebete na Nyangulu vilivyopo Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, mkoani Mbeya, alipokuwa akizindua miradi mbalimbali ya maendeleo iliyofadhiliwa kupitia Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bayoanuai Tanzania (SLR), unaotekelezwa chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais.

Akizungumza mbele ya wananchi, viongozi wa serikali za vijiji, wataalamu wa sekta mbalimbali pamoja na wanufaika wa miradi hiyo, Dkt. Muyungi alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwekeza nguvu kubwa katika utekelezaji wa miradi yenye tija kwa wananchi, hususan katika maeneo ya uzalishaji mali, uhifadhi wa mazingira na kuinua uchumi wa wananchi wa vijijini.

Alisema mafanikio ya miradi hiyo hayatategemea tu uwekezaji wa Serikali na washirika wa maendeleo, bali pia ushiriki wa wananchi katika kuitunza miundombinu iliyojengwa pamoja na kuhakikisha inatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

“Serikali inaendelea kuwekeza fedha nyingi katika kuboresha maisha ya wananchi kupitia miradi ya maendeleo.

Hata hivyo, ni muhimu kwa wanufaika kuhakikisha miradi hii inalindwa, inatunzwa na kuendelezwa ili iweze kudumu na kuendelea kuwa msaada katika kufikia azma ya taifa ya kuwa na uchumi wa kati wa juu ifikapo mwaka 2050,” alisema Dkt. Muyungi.

Akiwa katika Kijiji cha Matebete kilichopo Tarafa ya Ilongo, Kata ya Itamboleo, Dkt. Muyungi alizindua Mradi wa Kiwanda cha Kusindika Maziwa unaokadiriwa kugharimu zaidi ya shilingi milioni 200.

Mradi huo unatajwa kuwa miongoni mwa miradi muhimu inayolenga kuimarisha sekta ya mifugo na kuongeza thamani ya mazao ya mifugo kwa wananchi wa eneo hilo.

Fedha zilizotolewa kupitia mradi huo zimetumika kujenga miundombinu mbalimbali ya mifugo ikiwemo josho, kibanio, birika pamoja na kisima kirefu cha maji kwa ajili ya kunyweshea mifugo.

Aidha, fedha hizo pia zimetumika kujenga kiwanda cha kusindika maziwa kitakachosaidia kuongeza thamani ya maziwa yanayozalishwa na wafugaji wa eneo hilo.

Kwa mujibu wa taarifa ya wataalamu wa mradi huo, kisima kilichojengwa kinatarajiwa kuwa na uwezo wa kuzalisha na kuhifadhi maji lita 10,000 kwa siku, hatua ambayo itaondoa changamoto ya upatikanaji wa maji kwa mifugo iliyokuwa ikiwakabili wafugaji kwa muda mrefu.

Sambamba na hilo, kiwanda cha kusindika maziwa kinatarajiwa kuwa na uwezo wa kuhifadhi lita 500 za maziwa kwa siku, hali itakayosaidia kupunguza upotevu wa maziwa, kuongeza thamani ya bidhaa hiyo na kuwainulia kipato wafugaji wa eneo hilo.

Dkt. Muyungi alisema uwepo wa kiwanda hicho utasaidia pia kufungua fursa za ajira kwa vijana na wanawake huku ukichochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi katika maeneo ya vijijini.

“Miradi kama hii siyo tu kwamba inaleta maendeleo ya kiuchumi, bali pia inasaidia kuhifadhi mazingira kwa sababu wananchi wanapata shughuli mbadala za kujiongezea kipato bila kutegemea uharibifu wa mazingira,” alisema.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu huyo alitembelea Kijiji cha Nyangulu ambapo alizindua kiwanda cha kuchakata alizeti kilichojengwa kupitia mradi huo wa SLR.

Akiwa katika uzinduzi huo, aliwataka wananchi kuhakikisha wanatumia vizuri miundombinu hiyo kwa kuongeza uzalishaji wa alizeti na kuimarisha ushirikiano katika usimamizi wa kiwanda hicho.

Alisema uwepo wa kiwanda hicho utasaidia wakulima kupata soko la uhakika la zao la alizeti pamoja na kuongeza thamani ya mazao yao badala ya kuuza malighafi bila faida kubwa.

“Tunataka kuona wananchi wanazalisha kwa wingi, wanachakata na kuuza bidhaa zenye thamani kubwa zaidi. Hii ndiyo njia sahihi ya kujenga uchumi imara wa wananchi wetu,” alisisitiza.

Aidha, Dkt. Muyungi alibainisha kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha miradi ya maendeleo inayotekelezwa nchini inaleta matokeo chanya kwa wananchi na kusaidia kuondoa umasikini, huku ikizingatia uhifadhi endelevu wa mazingira.

Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bayoanuai Tanzania (SLR) ni miongoni mwa miradi inayolenga kuunganisha uhifadhi wa mazingira na shughuli za kiuchumi kwa wananchi, kwa kuhakikisha jamii zinanufaika moja kwa moja na rasilimali zinazowazunguka kupitia matumizi endelevu ya mazingira.

Habari

Settings