Dkt. Jafo: Serikali kuendelea kuzipa kipaumbele kampeni za upandaji miti

Mar, 18 2023

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dk. Selemani Jafo amesema Serikali itaendelea kuzipa kipaumbele kampeni za upandaji kwasababu zinatekeleza maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Amesema hayo wakati akizindua Kampeni ya ‘Play 2 Zero’ inayolenga kupanda miti kwa shule za msingi na sekondari ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi Machi 18, 2023 katika Shule ya Sekondari Minaki wilayani Kisarawe mkoani Pwani ambapo jumla ya miche 200 ya mipera imepandwa.

Dkt. Jafo amesema Amesema kuwa athari za mabadiliko ya tabianchi yamejidhihirisha wazi katika baadhi ya maeneo hapa nchini hali iliyosababisha wanyama kufa kutokana na ukame uliochangia kukauka kwa majani ya malisho.

Dkt. Jafo amebainishja kuwa kampeni hii itachagiza uhifadhi wa mazingira na kuwafanya wanafunzi kuwa na utamaduni wa kupanda miti kuanzia wakiwa wadogo, lengo ikiwa ni kuifanya Tanzania kuwa ya kijani na kuyahifadhi mazingira.

Katika kampeni hiyo ya ‘Play 2 Zero’ inayofanywa na taasisi ya African Lyon Foundation inalenga kupanda miti ya matunda 1600 katika shule nane, ambapo kila shule itapanda miti 200.

Amewaagiza walimu kuhakikisha miti inastawi katika shule zao kwani katika miti 200 kuna mingine ambayo inaweza isistawi vizuri au ikaishia njiani, hivyo ni matarajio kuwa miti 800 itakuwa imestawi vizuri,

“Shule zitakazofanya vizuri zitapata bonasi. Kuna kitengo cha ufuatiliaji na tathmini kikibaini shule fulani imefanya vizuri miti yao imestawi vizuri, lazima ipewe bonasi, nawaomba walimu msimamie vyema programu hii ya play 2 ziro,” amesisitiza.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Afrian Lyon Foundation, Rahim Kangezi, ameishukuru Serikali kuunga mkono kampeni hiyo ambayo inalenga kuwekeza katika jamii ambapo amemkabidhi Waziri Jafo ripoti mbili ambazo wameziandaa ikiwemo ya Kampeni ya Linda Tembo wetu na ya Chanjo ya Uviko 19.

Naye, Ofisa Maliasili kutoka Mkoa wa Manyara Michael Gwadu amesema mradi wa Play 2 Ziro ambao unajihusisha na michezo na uhifadhi wa mazingira, una lengo la kupunguza gesi joto kufikia ziro, hivyo wanafunzi watacheza na hapo hapo kulinda mazingira.

Amesema kuwa mradi huo awamu ya kwanza unatekelezwa katika mikoa nane, ambayo ni Tabora, Pwani, Morogoro, Lindi, Tanga, Manyara, Singida, Dodoma na Dar es Salaam.

Settings