Dkt. Jafo azihimiza taasisi za elimu kupanda miti kwa wingi

Apr, 21 2024

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira0 Mhe. Dkt. Selemani Jafo amezitaka taasisi za elimu nchini kuongeza kasi ya upandaji miti kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Dkt. Jafo ametoa wito wakati akihutubia kwenye mahafali ya kwanza ya kidato cha sita ya Shule ya Fountain Gate Dodoma, Aprili 20, 2024 ambapo ameonesha kuridhishwa na namna wanafunzi wa shule hiyo wanavyojikita katika elimu ya mazingira.

Amesema mabadiliko ya tabianchi ni ajenda ambayo athari zake ni kubwa zinazosababisha mvua zisinyeshe kwa wakati au kunyesha kwa kiwango kisichotarajiwa hali inayosababisha mafuriko.

Halikadhalika, Dkt. Jafo ametanabahisha kuwa mabadiliko ya tabianchi husababisha baadhi ya maeneo kukabiliwa na ukame uliopitiliza na hivyo kuchangia wanyama kufa na mazao kukauka.

Amesema kutokana na changamoto hiyo, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, Januari 20, 2022 ilizindua Kampeni ya ‘Soma na Mti‘ inayomtaka kila mwanafunzi wa shule ya msingi, sekondari na chuo kupanda mti.

“Nimefurahi sana kusikia vijana hapa shuleni wakati wa risala yao wanazungumzia ajenda ya mabadiliko ya tabianchi, hii maana yake sasa tutakuwa na taifa la vijana ambao wanajua athari za mabadiliko ya tabianchi na kuweza kusambaza elimu hiyo kwa wengine,“ amesema.

Kwa upande mwingine, Waziri Dkt. Jafo amesema Serikali imeweka mazingira wezeshi kwa wanaotaka kuwekeza katika elimu kwa ajili ya kuandaa vijana kusomea fani mbalimbali katika vyuo na hatimaye walitumike taifa.

Settings