Dkt. Jafo ahimiza taasisi zipande miti kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi

Apr, 27 2024

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amezitaka taasisi mbalimbali kuongeza kasi ya upandaji wa miti katika maeneo yao ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Amesema hayo wakati akishiriki zoezi la kupanda miti ya matunda katika ofisi za Redio Jamii za Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) mkoani Arusha leo tarehe 27 Aprili, 2024.

Amelipongeza shirika hilo kwa kuendesha kampeni ya upandaji miti katika maeneo mbalimbali nchini ambapo tangu mwaka jana wamefanikiwa kupanda miti 3,000 ikiwa ni katika kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Waziri Dkt. Jafo amesema kuwa kampeni ya upandaji wa miti inayoendeshwa na shirika hilo la umma ina mchango mkubwa katika hifadhi ya mazingira hususan katika maelekezo ya kila halmashauri kupanda miti milioni 1.5 kila mwaka.

"Niwashukuru TBC kwa sababu mlianza zoezi la Mti wa Mama nawapa 'big up' sana kwasababu mmeonesha mfano na nadhani wengine wanatakiwa waige mfano kama huu, kila taasisi," amesema Dkt. Jafo

Amesema wananchi wana kila sababu ya kuendelea kushiriki katika zoezi la kupanda miti na kwamba hadi kufikia hivi sasa tayari takriban 266 imepandwa kati ya 276 ambayo ni malengo ya Serikali kwa kila halmashauri.

Halikadhalika, ametoa wito kwa wananchi kutumia mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini kupanda miti akisisitiza miti inayopandwa itunzwe na kutoruhusu mifugo kuivamia kwani kufanya hivyo zoezi la upandaji wa miti litakuwa halkina maana tena.

Kwa upande wake Mkuu wa Kanda ya Kaskazini TBC Bi. Anna Kwambaza amesema miti iliyopandwa leo ni 25 ikiwemo ya matunda 15 ambayo ni miembe, miparachichi, michungwa na ya kivuli.

Amesema miti ina faida nyingi na ndio maana mkoani Arusha kuna hali nzuri ya hewa kutokana na utunzaji wa mazingira na kuwa shirika linaendesha kampeni hiyo ya kipekee ili kutunza mazingira.

Bi. Anna ameongeza kuwa kwa kupanda miti hiyo wanawaelimisha pia wananchi hususan majirani wanaozunguka ofisi za shirika hilo kwani wanajifunza.

Nae Meneja wa Kanda ya Kaskazini wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Bw. Benjamin Doto amesema miti ni kama mapafu ya dunia ambayo tukiitunza tunaiweka katika hali nzuri.

Tunapoendelea kuiotesha na kuitunza miti tunaifanya dunia kuwa katika mahali pazuri pa kuishi na hatua hiyo inasaidia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Pia, meneja huyo amewasisitiza wananchi kutumia mvua zinazoendelea kunyesha kwa ajili ya kupanda miti kwani ni wakati ambao maji yanapatikana kwa urahisi.

Settings