Tanzania yakabidhi kiti uenyekiti Mawaziri Ziwa Tanganyika

Dec, 10 2022

Serikali ya Tanzania imeikabidhi Burundi kiti cha uenyekiti wa Mawaziri waliopo katika Mkataba wa Kikanda wa Usimamizi Endelevu wa Ukanda wa Ziwa Tanganyika na kusisitiza Kiswahili kitumike kama lugha kuu ya mawasiliano katika mikutano yote itakayofanyika.

Hayo yamefanyika wakati wa Mkutano wa 10 wa Mawaziri hao uliofanyika jana jijini Bujumbura nchini Burundi baada ya Tanzania kumaliza muda wa uenyekiti uliodumu kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Akizungumza wakati wa mkutano huo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo alisema Tanzania inashiriki katika shughuli zote zinazolenga kuhakikisha usimamizi endelevu wa rasilimali za ziwa hilo.

Pia, alisema Tanzania imedhamiria kushirikiana na nchi wanachama ambazo ni Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Zambia katika utekelezaji wa programu za kikanda zinazolenga kulinda rasilimali za pamoja za Ziwa Tanganyika na kuboresha maisha ya watu katika bonde hilo.

Dkt. Jafo alisema Ziwa Tanganyika ni rasilimali muhimu kwa wananchi takriban milioni 10 wa ukanda huo wanaolizunguka hivyo zinahitajika juhudi za pamoja katika kulilinda.

“Waheshimiwa mawaziri, mazingira tunayoishi yanabadilika haraka sana na shughuli za binadamu zinatumia maliasili za dunia kwa kasi ya kutisha na kuharibu mifumo ikolojia. Inakadiriwa kuwa zaidi ya viumbe 22,000 wako hatarini kutoweka ikiwa ni pamoja na baadhi ya viumbe katika Ziwa Tanganyika,” alisema.

Hivyo, alitoa wito kwa Mawaziri hao kutoka nchi wanachama kuungana kwa pamoja kujadili namna bora ya kulinda Ziwa Tanganyika kwa leo na kizazi kijacho huku akisisitiza umuhimu wa kuweka utaratibu wa muda mrefu wa ufadhili wa programu ya maendeleo ya Ukanda ya Ziwa Tanganyika.

Ujumbe ulioshiriki katika Mkutano huo uliwashirikisha pia Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Dkt. Switbert Makama, Mkurugenzi wa Mazingira Dkt. Andrew Komba, Afisa Mazingira Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Deogratius Nyangu na uwakilishi wa Wizara ya Fedha na Mipango pamoja ba Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Settings