Mkutano wa COP30 wailetea neema Tanzania, yapata fedha

Dec, 17 2025

Tanzania inatarajia kunufaika na ufadhili wa Dola za Marekani milioni 447.12 na Euro 500,000kutokana na ushiriki wake katika Mkutano wa 30 wa Nchi Wanachama wa Mkataba Mabadiliko ya Tabianchi (COP30) uliofanyika Belem, Brazil hivi karibuni.

Pia, Tanzania itapata kiasi cha Dola milioni 5 hadi 20 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kupitia Mfuko wa Upotevu na Hasara.

Hayo yamebainishwa na Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Prof. Peter Msoffe leo Desemba 17, 2025 jijini Dar es Salaam wakati akifungua Mkutano wa Wadau wa Kupokea Taarifa ya Ushiriki wa Tanzania katika Mkutano COP 30, kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu Wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja.

Prof. Msoffe ameeleza kuwa lengo la mkutano huo kuangaza na kujadili fursa mbalimbali katika kuuisaidia jamii katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kupitia miradi ya mazingira inayotekelezwa na Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais pamoja na wadau.

Alisema ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo wa kila mwaka ulikuwa na umuhimu wa pekee, kwani uliiwezesha nchi kuwasilisha msimamo wake pamoja na kuongoza bara la Afrika katika majadiliano ya mabadiliko ya tabianchi, hususan katika eneo la uhimilivu, ambapo mwaka huu Tanzania ilishiriki ikiwa Mwenyekiti wa Kundi la Majadiliano la Wataalamu wa Afrika.

Aliongeza kuwa Tanzania imeendelea kuimarisha hadhi yake kimataifa kupitia nafasi yake kama Mwenyekiti wa Kundi la Majadiliano la Afrika (AGN) ambapo imewezesha kujadiliwa na kukubalika kwa ajenda ya Nishati Safi ya kupikia, kukubalika kwa hoja ya upatikanaji wa umeme wa bei nafuu kwa watu wote (Mission 300).

“Tumeona hatua nzuri kupitia mkutano huo kama vile Tanzania kufikia maamuzi ya nchi wanachama, kuwezesha Ofisi ya Kanda ya Santiago Network on Loss and Damage ambayo itafunguliwa Dar es Salaam. Tukumbuke hii ni nafasi ya nishati safi ya kupikia kimataifa ni ajenda inayopewa nguvu na uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema.

Kwa upande wa Biashara ya Kaboni, Prof. Msoffe alibainisha kuwa imefanikiwa kupata ufadhili wa misitu ya kitropiki kupitia Mfuko wa Tropical Forest Forever Facility (TFFF).

Ili kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuimarisha usimamizi wa biashara ya kaboni, alitoan wito kwa sekta binafsi kuongeza ushiriki kwenye masoko ya biashara hiyo kwani ina uwezo mkubwa wa ubunifu.

Halikadhalika, aliwaomba wadau hao kuendelea kuandaa miradi ya kimkakati itakayoweza kufadhiliwa chini ya utekelezaji wa Dira 2050 na maamuzi ya COP30, hususan miradi ya uhimilivu, mifumo ya tahadhari mapema, nishati safi ya kupikia na teknolojia, biashara ya kaboni, uhufadhi na usimamizi wa misitu, maji, kilimo na taka.

Kwa upande wake Mshauri wa Rais katika masuala ya Mabadiliko ya Tabianchi na Mazingira Dkt. Richard Muyungi alisema kuwa miongoni mwa agenda kuu za katika mkutano huo Tanzania iliwasilisha ni pamoja na kupata fedha za mabadikliko ya tabianchi.

Dkt. Muyungi ambaye ni Mwenyekiti wa AGN alisema nchi zilizoendelea zinawajibika kutimiza ahadi zao za kutoa fedha na sio mikopo hizo kwa nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania.

Dkt. Mayungi amesema mkutano huo ulijikita katika ajenda mbili kuu, ikiwemo ajenda rasmi chini ya Umoja wa Mataifa na majadiliano ya kuendeleza makubaliano yaliyopo, ambapo Afrika ilisisitiza haki ya kupata rasilimali za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa mfumo wa ruzuku badala ya mikopo, ikizingatiwa kuwa athari hizo zimesababishwa zaidi na nchi zilizoendelea.

Ameeleza kuwa mafanikio makubwa yalipatikana baada ya kukubaliana kuimarishwa kwa mifuko ya kimataifa ikiwemo Green Climate Fund, Adaptation Fund, LDC Fund na Loss and Damage Fund, ambapo mfuko wa hasara na uharibifu tayari umefikisha zaidi ya dola milioni 800.

Kuhusu uhimilivu, Dkt. Mayungi amesema mkutano huo ulipitisha viashiria vya kimataifa vya kupima namna nchi zinavyokabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, hususan kwa jamii za vijijini, akieleza kuwa ndani ya miaka miwili nchi zitapaswa kuwasilisha taarifa kupitia mfumo wa Global Vulnerability Indicators.

Akizungumzia manufaa ya moja kwa moja kwa Tanzania, Dkt. Mayungi amesema nchi imepata nafasi ya kuanzisha Kituo cha Vijana cha Afrika kwa ajili ya mafunzo ya mabadiliko ya tabianchi pamoja na ofisi ya uratibu wa masuala ya majanga yanayotokana na tabianchi chini ya Umoja wa Mataifa, akisisitiza kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya uongozi thabiti wa nchi na ushiriki wake mzuri katika majadiliano ya kimataifa.

Settings