Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango ametoa wito kwa Watanzania kuhakikisha matumizi adili ya rasilimali za nchi kama njia ya kumshukuru Mungu.
Makamu wa Rais ametoa wito huo alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Jubilei ya Miaka 25 ya Uaskofu wa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es salaam Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi (OFMCap) iliyofanyika Parokia ya Bikira Maria wa Fatima – Msimbazi Centre Dar es Salaam.
Amesema Viongozi na Watumishi wa serikali wanayo nafasi kubwa ya kusimamia matumizi ya rasilimali za nchi na kuwaongoza watanzania katika ni kuhakikisha mazingira mazuri ya nchi yanatunzwa na kurekebishwa pale ambapo tayari yameharibiwa kwa uchomaji moto hovyo wa misitu, uharibifu wa vyanzo vya maji, uchafunzi wa mazingira ya mito na bahari.
Amesema ni vema kumshukuru Mungu kwa neema zake kwa kusali au kumtolea maombi ya shukurani pamoja na kutimiza wajibu wa kutunza na kustawisha fadhila zote ambazo Mungu ametutendea. Amesema Watanzania wanaweza kumshukuru Mwenyezi Mungu vizuri zaidi kwa kuthamini na kuitunza nchi nzuri ya Tanzania tuliyojaaliwa.
Amewasihi Watanzania kuwajibika kumshukuru Mungu kwa amani na mtangamano katika Taifa kwa miaka 63 ya uhuru na kuwezesha kuishi kwa ushirikiano baina ya watu wa imani, rangi, kabila na itikadi za kisiasa tofauti tofauti. Amesema ni baraka za kushukuru kwa kuwa na Taifa lenye ardhi nzuri, maziwa, mito na vijito, bahari, misitu, mabonde na milima, madini ya aina mbalimbali, wanyama wa kufugwa na wa porini, ndege, wadudu, neema ya mvua na hali ya hewa nzuri.
Makamu wa Rais amesema ni wajibu kushukuru kwa kuwa shukurani inafungua milango iliyofungwa hususan pale binadamu anapokabiliwa na ugumu wa maisha, magonjwa, biashara kudorora, changamoto za kazi na mara zote Mungu humpa anayeshukuru zaidi ya kile anachoshukuru kukipokea kwani shukurani inaonesha kwamba mtoa shukurani anatambua mchango wa mwenyezi Mungu katika maisha yake.
Makamu wa Rais amempongeza Askofu Mkuu Jude Ruwa’ichi kwa kutimiza miaka 25 ya Uaskofu na kukumbuka kumshukuru Mwenyezi Mungu, ambaye amemjalia neema nyingi na kumwezesha kutekeleza utume wake kikamilifu kwa miaka yote 43 ya Upadre wako ambayo 25 amekuwa Askofu. Aidha amempongeza kwa mchango mkubwa katika kuanzisha Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT) na Vyuo Vikuu Vishiriki vya Mtwara, Songea na Moshi.