Waziri Tax aipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kutoa elimu ya mazingira

Jan, 29 2024

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Stergomena Tax ameipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa zoezi la upandaji miti linaloendelea mkoani Dodoma tangu Januari 25, 2024 kuelekea Maadhimisho yai Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Mhe. Stergomena amesema hayo alipowaongoza viongozi mbalimbali katika zoezi la upandaji miti katika eneo la Makao Makuu ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) mkoani Dodoma leo Januari 29,2024.

Amesema watu wengi wananufaika na elimu ya mazingira inayotolewa na Idara ya Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais jambo ambalo ni la kujivunia na wasisite kuzidi kutoa elimu kwa jamii kuhusu utunzaji wa mazingira hasa katika kupanda na kutunza miti.

“Jamii itambue hili ni jambo la wote hivyo mtu au watu wanapofanya jambo lolote kama vile kusherehekea siku ya kuzaliwa basi wanapokutana wapande miti ili iwe kumbukumbu zaidi kwa vizazi vijavyo.

Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis amesema upandaji miti ni moja ya shughuli muhimu katika maisha ya binadamu zaidi ukizingati kilio cha dunia kwa sasa ukiachilia mbali maradhi, dunia kwa sasa imejielekeza katika utunzaji wa mazingira na kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

“Athari nyingi za uharibifu wa mazingira hutokana na shughuli za binadamu kama vile uchimbaji madini, ufugaji, uchomaji misitu, ukataji miti, shughuli za kilimo na uvuvi.

“Tunashukuru namna ambavyo uongozi wa JKT ulivyounga mkono shughuli hii ambayo inaratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais ambayo iliasisiwa na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tangu mwaka 2017 alipoizindua kampeni hii akiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema Mhe. Khamis.

Ameongeza kuwa upandaji wa miti ni ibada kwa kuwa miti inayopandwa leo itanufaisha wengi kwa sasa na baadaye kwa kuitumia katika kivuli kama ilivyo miti inayotumika sasa ilipandwa na watu hapo nyuma ndio inanufaisha watu sasa, hivyo kuna wajibu wa kurithisha jamii katika zoezi hilo.

Settings