Waziri Pindi: Wakulima acheni kuchoma moto mashamba

Jan, 11 2023

Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amewataka wakulima kuacha mara moja tabia ya kuandaa mashamba kwa kuchoma moto kwani inaathiri uoto wa asili, amewataka watumie njia mbadala ili kuendelea kuhifadhi misitu.

Amesema hayo leo Januari 11, 2023 wakati akiongoza zoezi la upandaji miti katika Bwawa la Swaswa, Ipagala jijini Dodoma ikiwa ni muendelezo Wiki ya Maadhimisho ya miaka 59 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

Dkt. Chana amesema athari za moto ni kubwa kwani unasambaa kulingana na uelekeo wa upepo na kwenda maeneo ambayo hayakukusudiwa kuchomwa hivyo inasababisha uharibifu wa misitu.

Aidha, amewataka wafugaji kuacha tabia ya kuingiza mifugo katika hifadhi ya misitu na hasa katika miti hiyo inayopandwa kwa sasa kwani mifugo inachochea jangwa na kupelekea athari ambazo zinafika mbali zaidi na kupelekea hata kutokea kwa upungufu wa maji kwani kunakuwepo na uharibifu wa vyanzo vya maji.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) Bw. Abdallah Hassan Mitawi amesema kuwa mapinduzi ya Zanzibar ndiyo kielelezo cha Muungano, Uhuru na Mshikamano wa Tanzania na imeonekana ni vyema kusherehekea kwa kupanda miti ili kuendelea kukijanisha Dodoma.

Mitawi amesema kuwa wamedhamiria kupanda miti 5,000 ndani ya siku tatu katika Jiji la Dodoma jambo ambalo litaacha kumbukumbu ya kudumu ya miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar

"Kupanda miti sio kazi ila kazi kubwa ni kutunza miti hii ikue kwani baadhi ya watu hawana desturi ya kutunza miti hivyo niwatake wananchi kutunza miti na kuacha tabia ya kuachia mifugo kula miti waache mara moja," amesema Mitawi

Settings