Waziri Jafo awakaribisha Shirika la Mazingira Korea kuwekeza teknolojia usimamizi taka

Oct, 29 2023

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Shirika la Mazingira la Korea (KEPO) Dkt. Yoon, Young-bong jijini Incheon, Korea Kusini.

Katika mazungumzo yao Dkt. Jafo ameeleza nia ya Tanzania katika kuanzisha ushirikiano kwenye sekta ya utunzaji wa mazingira hususani katika teknolojia ya usimamizi wa taka.

Katika kikao hicho akiwa na Balozi wa Tanzania nchini Korea Kusini Mhe. Togolani Mavura, viongozi hao wamejadili kuhusu kubadilishana uzoefu wa kisera katika upande wa mazingira.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa shirika hilo Dkt. Young-bong amemueleza Waziri Dkt. Jafo kuwa wako tayari kushirikiana na Tanzania katika usimamizi wa taka.

Hivyo, viongozi hao wamekubaliana kuendeleza mazungumzo katika kuelekea hatua za utekelezaji wa ushirikiano huo ambao unatarajiwa kusaidia katika utunzaji wa mazingira nchini Tanzania.

Serikali kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo imeendelea kuibua miradi ya kuziwezesha Mamlaka za Serikali za Mitaa kusimamia taka nchini Tanzania.

Amesema Ofisi ya Makamu wa Rais imeandaa Mpango Kabambe wa Hifadhi ya Mazingira (2022 – 2032) ambayo pamoja na mambo mengine changamoto za hifadhi ya mazingira na hatua za kukabiliana nazo zimeainishwa.

Hali kadhalika Ofisi kwa kushirikiana na wadau imeandaa Mwongozo wa Usimamizi Endelevu wa Taka kwa kuzingatia dhana ya ‘Punguza Uzalishaji wa Taka, Tumia tena na Rejereza‘.

Katika ziara hiyo ya kikazi ya kuimarisha ushirikiano katika masuala ya mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, Waziri Dkt. Jafo ameambatana na Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Sheria Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Dustan Shimbo.

Itakumbukwa kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuimarisha diplomasia na mataifa mbalimbali duniani.

Settings