Wananchi watakiwa kuendeleza misitu kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi

Feb, 09 2022

Waziri Dkt. Ndumbaro: Wananchi wafanye matumizi endelevu ya misitu badala ya kukata miti ovyo hali inayoweza kusababisha mabadiliko ya tabianchi.

Dkt. Ndumbaro ametoa rai hiyo jana wakati akizungumza na wadau mbalimbali mara baada ya kushiriki zoezi la upandaji miti katika eneo la Iyumbu jijini Dodoma.

Alibainisha kuwa asilimia 54 ya eneo la nchi yetu ambayo ni sawa na hekta 400 ni misitu, hivyo kila mwananchi analo jukumu la kuitunza na kuendelea kupanda miti mingine ili iendelee Tanzania iendelee kuwa ya kijani kuleta faida.

“Ndugu zangu faida za misitu tunazijua, misitu ni mali kwasababu watu wanaishi Mafinga mkoani Iringa na maeneo mengine misitu ndio biashara yao n ahata kule nchini Norway misitu inachangia sana kwenye GDP,” alisema.

Aidha, Waziri Dkt. Ndumbaro aliongeza kuwa kutokana na umuhimu wa misitu hiyo asilimia 3.5 ya Pato la Taifa (GDP) inachangiwa na sekta hiyo hapa nchini hivyo alisisitiza umuhimu wa kuilinda.

Hivyo, aliipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuratibu Wiki ya Mazingira kuelekea kilele cha uzinduzi wa Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021 na kushiriki zoezi la upandaji miti kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika msimu huu wa mvua waliotoa miche ya miti mbalimbali ambayo imepandwa leo katika eneo la Greenpark, Iyumbu jijini Dodoma.

Alisema miti hiyo itasaidia kukabiliana na madhara yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi ambayo yameendelea kushuhudiwa kutokana na mabadiliko yake kuja na athari hasi nyingi zikiwemo kuongezeka kwa joto duniani, kuongezeka kwa baridi, pamoja na kubadilika kwa misimu ya hali ya hewa.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Mary Maganga alitoa wito kwa wananchi kupanda miti katika maeneo yao ili kuendelea kuifanya nchi kuwa ya kijani na mfano wa kuigwa.

Bi. Maganga alisema zoezi la upandaji ni kielelezo cha kutoa hamasa na kuhamasisha maeneo mengine nchi nzima kupata uelewa kuhusu dhana nzima ya kuifanya nchi nzima kuwa ya kijani nay a mfano kupitia kampeni ya Kijanisha Dodoma.

Pia aliwashukuru wadau waliojitokeza katika zoezi hilo na wadau mbalimbali wa mazingira hatua itakayoleta hamasa kwa wananchi ili waweze kufanya shughuli za upandaji miti na kuhifadhi mazingira kuwa sehemu ya maisha yao.

Nae Kamishna wa Uhifadhi kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Pro. Dos. Santos Silayo alisema nchi yetu imejaliwa kuwa na misitu ya aina mbalimbali ikiwemo ya kupanda na kuota.

Prof. Silayo aliwataka wananchi kuwa na utamaduni wa kuitunza misitu iliyopo kwani ina mchango mkubwa katika sekta ya viwanda ambayo imekwa kwa kasi kubwa hapa nchini.

Aliongeza kwa kusema kuwa katika miaka mitatu sekta iliyopita tulishuhudia viwanda takriban 800 vikiwemo vya kati na vikubwa vikianzishwa sambamba na ukuaji wa teknolojia huku akitolea mfano wa nguzo za umeme zinazozalishwa hapa nchini kutokana na misitu.

Kamishna huyo alisema Ukuaji wa viwanda umekwenda kwa kasi kubwa na hata tunashuhudia viwanda vya mkaa mbadala ambavyo vyote vinaleta mchango mkubwa katika kuhifadhi mazingira.

Settings