Wanachuo wahimizwa kuendelea kuhifadhi mazingira

Jan, 07 2023

Wanafunzi wa vyuo nchini wametakiwa kuendelea kuwa mstari wa mbele katika utekezaji wa shughuli mbalimbali za kuhifadhi na kulinda mazingira ili kupambana na mabadiliko ya tabianchi.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Andrew Komba wakati akishiriki katika zoezi la usafi wa mazingira katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma lililoandaliwa na Jumuiya ya Wanafunzi Taasisi za Elimu ya Juu (TAHLISO) leo Januari 07, 2023.

Dkt. Komba ambaye amemwakilisha Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Dkt. Switbert Mkama amesema kuwa zoezi hilo la usafi ni sehemu ya kuungano mkono utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 2021.

Amewapongeza wanafunzi hao wa vyuo kwa kuandaa zoezi hilo la usafi ikiwa ni katika kuunga mkono juhudi za Serikali za usafi na uhifadhi wa mazingira ambapo kuanzia Januari 10, 2023 inatarajia kupanda miti katika Jiji la Dodoma.

“Kama mnavyofahamu Serikali ilishautenga Mji wa Dodoma kuwa wa mfano katika masuala ya mazingira hivyo tunahakikisha tunapanda miti ya kutosha na nyie hapa leo mmeonesha mfano kwa kufanya usafi hospitalini hapa,” amesema Dkt. Komba.

Mkugenzi huyo ameongeza kuwa ni wakati muafaka kwa wanafunzi wa vyuo kuwarithisha wadogo zao njia za kutunza mazingira kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Afya Mazingira Hospitali ya Mkoa wa Dodoma Paul Mageni amesema katika kuunga mkono Serikali wameanzisha bustani ya miti katika eneo la hospitali hiyo.

Aidha, Mageni amesema miti iliyopandwa mbali ya kuhifadhi mazingira lakini pia inawasaidia wananchi wanaopata huduma hospitalini hapo kupata hewa nzuri na matunda.

Kwa upande wao viongozi wa TAHLISO kutoka Tanzania Bara na Visiwani wametoa pongezi kwa uongozi wa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma wa kuwapa wasaa wa kufanya usafi katika eneo hilo.

Settings