Wadau wa maendeleo watakiwa kuchangamkia fursa za uchumi wa buluu

Sep, 10 2025

Wadau wa maendeleo wametakiwa kuchangamkia fursa zilizopo katika uchumi wa buluu na kutoa mapendekezo yatakayosaidia Serikali na sekta binafsi kuchukua hatua zitakazochangia kukuza pato la taifa kupitia sekta hiyo.

Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Abdallah Hassan Mitawi wakati akifungua Kongamano la Uchumi wa Buluu jijini Dar es salaam leo Septemba 10, 2025.

Amesema katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imetambua uchumi wa buluu kama sekta mojawapo ya mageuzi na kuiwekea mikakati mbalimbali itakayowezesha kuinyanyua na kuitumia kama sekta chagizo kwa sekta zingine kama ikitumika ipasavyo

Amesema kuwa vijana, wanawake na wadau wa sekta binafsi wana nafasi kubwa katika kuchangia uchumi wa buluu hivyo wanapaswa kupewa kipaumbele katika sera, mafunzo na uwezeshaji wa kifedha ili waweze kushiriki kikamilifu na kwa tija.

Bw. Mitawi ameongeza kuwa ushirikiano kati ya nchi jirani na taasisi za kimataifa ni muhimu kwani bahari haina mipaka hivyo mafanikio katika sekta hii yanahitaji mshikamano wa kitaifa, kikanda na kimataifa.

Aidha, amesisitiza kuwa uchumi wa buluu ni eneo lenye fursa kubwa ambazo hazijatumika na zikitumika ipasavyo zitakuwa ni uti wa mgongo wa mageuzi ya maendeleo ya taifa kutokana na kuwepo kwa maeneo makubwa ya vyanzo vya maji.

”Sote tunatambua kuwa uchumi wa buluu unapatikana kupitia mito, bahari, maziwa, misitu na ardhi oevu nchini ambayo yakitumika ipasavyo yataongeza ajira, kukuza biashara, kuimarisha usalama wa chakula hivyo kuboresha maisha ya wananchi,” amesema. Bw. Mitawi.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uchukuzi Bw. Shomari Shomari ameelezea nafasi kubwa ya sekta ya usafirishaji na maboresho ya miundombinu ya bandari katika kuimarisha uchumi wa buluu.

Amebainisha kuwa miradi mikubwa ya kisasa ya reli, maboresho ya bandari na udhibiti wa usafiri na usalama wa majini ni nyenzo muhimu katika kufungua fursa za uchumi wa buluu ikiwemo kukuza biashara na ajira kwa Watanzania

Awali, Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) Prof. Tumaini Gurumo ameeleza majukumu na mchango wa chuo hicho katika sekta nzima ya uchumi wa buluu.

Amesema kuwa chuo hicho kinatoa mafunzo na tafiti mbalimbali zinazohusiana na bahari na usafirishaji ambao una mchango mkubwa katika sekta ya uchumi wa buluu.

Pia amefafanua dhumuni la kongamano la uchumi wa buluu kwa mwaka 2025 ambalo ni kuhamasisha uwekezaji, ushirikiano na utafiti zaidi katika maeneo ya uvuvi, usafiri wa majini, nishati jadidifu kutoka baharini ,utunzaji wa mazingira sambamba na kuangazia changamoto zilizopo na kutafufuta ufumbuzi wa pamoja.

Kongamano hilo la siku mbili limeandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Wizara ya Uchukuzi na Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) ambapo linatarajiwa kuhitimishwa Septemba 11, 2025.

Settings