Tanzania inaweza kunufaika na takriban shilingi trilioni 2 kutokana na uwekezaji wa miradi mbalimbali ya ukiwemo uzalishaji wa umeme na teknolojia ya kuzalisha maji inayozingatia utunzaji wa mazingira.
Hayo yamebainika wakati wa kikao cha Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya CC Airwell ya Austria Bw. Wolfgang Fuchs kwa lengo la kutambulisha teknolojia hiyo, leo tarehe 26 Juni, 2024.
Katika mazungumzo yao, Dkt. Jafo ameipongeza kampuni hiyo kwa nia yake ya kushirikiana na Serikali kuwekeza nchini na pia kwa kuja na teknolojia mpya ya kuzalisha maji inayozingatia utunzaji wa mazingira.
Ameihakikishia kampuni hiyo ushirikiano wa kutosha ili azma yake katika uwekezaji nchini iweze kufanikiwa na hivyo kuwasaidia wananchi kupata huduma ya maji wakati huo mazingira yanahifadhiwa.
Pamoja na kufuata kanuni na taratibu za nchi, pia Waziri Jafo alimuelekeza mkurugenzi huyo awasilishe maombi hayo rasmi katika Ofisi ya Makamu wa Rais pamoja na taasisi za Serikali zenye majukumu ya kuendeleza uwekezaji na biashara kwa ujumla.
Awali katika maelezo yake, Bw. Fuchs katika maelezo yake alisema teknolojia hiyo inaweza kuzalishaji hadi lita bilioni 1.7 za maji ya kunywa kila siku na kukuza ukijani bila umwagiliaji hivyo utakuwa na manufaa kimazingira.
Alitaja manufaa mengine ni uboreshaji wa miundombinu, ajira na uzalishaji wa umeme ambacho kiasi kitatumika katika kuendelesha shughuli za kampuni hiyo na kuwanufaisha wananchi.
Halikadhalika, mkurugenzi huyo amesema pamoja na teknolojia hiyo wanaangalia namna ya kuwekeza katika biashara ya kaboni hapa nchi ambayo mapato yatanufaisha vijiji vyenye hifadhi ya misitu.