UNEP yaombwa kuendelea kuipa Tanzania fedha za utekelezaji wa miradi ya mazingira

Feb, 01 2024

Shirika la Usimamizi wa Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) limeombwa kuendelea kutoa kipaumbele kwa Serikali ya Tanzania kupata fedha za utekelezaji miradi ya kukabiliana na athari za uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi.

Ombi hilo limetolewa na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Mary Maganga katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Kaimu Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Kemilembe Mutasa wakati wa Kikao cha Uratibu wa Tathimini ya Miradi ya Mazingira inayosimamiwa na UNEP nchini.

Amesema UNEP imeendelea kuwa mshirika wa maendeleo na Tanzania kupitia kufadhili miradi mbalimbali ikiwemo Mradi wa Hifadhi ya Ardhi ya Bonde la Ziwa Nyasa, Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bioanuai (SLR) na Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa Kutumia Mfumo wa Ikolojia Vijijini (EBBAR).

Maganga alisema kutokana na mafanikio yaliyopatikana katika miradi hiyo, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imewasilisha maandiko ya miradi mipya ya vipaumbele inayohitaji fedha zaidi kwa ajili ya kuunga jitihada za kimataifa za mapambano dhidi ya uharibifu wa mazingira na athari za mabadiliko ya tabianchi.

“Tunaishukuru UNEP kwa ushirikiano wa karibu na Tanzania katika jitihada za pamoja za kukabiliana na athari za uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi ili kuhakikisha jamii yetu na dunia kwa ujumla inaendelea kubaki salama,” alisema Maganga.

Aliongeza kuwa Tanzania ni nchi chache duniani zilizobarikiwa kuwa na rasilimali nyingi za asili ikiwemo misitu ya asili, mito, maziwa na bahari ambapo maeneo hayo yametengwa kwa ajili ya manufaa ya wananchi na dunia kwa ujumla na kupitia mikataba na itifaki za uhifadhi na usimamizi wa mazingira.

Alisema kutokana na umuhimu wa rasilimali hizo, Tanzania imeendelea kupiga hatua kubwa katika kusimamia na kutekeleza miradi ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi kwa kuimarisha ushirikiano na wadau pamoja na washirika wa maendeleo ili kufikia malengo ya kitaifa, kikanda na kimataifa.

Maganga alisema, Ofisi ya Makamu wa Rais pia imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuhuisha Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021 kwa kuboresha mpango mkakati, kanuni na miongozo mbalimbali ili kwenda sambamba na utekelezaji wa program na vipaumbele mbalimbali vya Serikali.

Aliongeza kuwa kutokana na kuhuisha Sera, Sheria na Kanuni za uhifadhi na usimamizi wa mazingiera, Tanzania imeweza kupiga hatua kubwa katika kubaini na kuibua fursa ya shughuli za kijamii na kiuchumi kwa wananchi kupitia raslimali za ardhini na baharini ikiwemo kuandaa Rasimu ya Sera ya Taifa ya Uchumi wa Buluu ya mwaka 2023.

Aidha ili kutekeleza vyema miradi hiyo, Maganga ameiomba UNEP kuandaa mpango wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wataalamu kutoka taasisi za Serikali na sekta binafsi katika kusimamia na kutekeleza miradi ya kimkakati ikiwemo fursa ya biashara ya kaboni.

Maganga aliihakikishia UNEP kuwa Tanzania itaendelea kuwa mstari wa mbele katika uhifadhi wa mazingira ikiwemo kuendelea kuhamasisha kampeni ya kupanda miti nchi nzima, utunzaji wa bioanuai, kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala, pamoja na utunzaji wa vyanzo vya maji.

Kwa upande wake, Mshauri wa Rais Masuala ya Mabadiliko ya Tabianchi na Mazingira Dkt. Richard Muyungi aliishukuru UNEP kwa kuendelea kuiwezesha Tanzania kupata fedha za utekelezaji wa miradi ya mazingira na kuliomba Shirika hilo kuanzisha ofisi yake nchini Tanzania ili kuongeza kasi ya ufuatialiji na utekelezaji wa miradi hiyo.

Aliitaja moja ya mradi uliotekelezwa na UNEP ni pamoja na Mradi wa kujenga uwezo wa Kuhimili Athari za Mabadiliko ya Tabianchi katika maeneo ya ukanda wa Pwani (LDCF) uliotekelezwa na Ofisi ya makamu wa Rais katika maeneo ya Bagamoyo, Pangani, Rufiji na Zanzibar na unafadhiliwa na Mfuko wa Dunia wa Mazingira (GEF).

Aliongeza kuwa fedha za Mradi huo zilitolewa na UNEP ikiwa ni pamoja na ushauri wa kitaalamu na usimamizi wa fedha ambapo utekelezaji wa Mradi huu ulianza mwaka 2013 na kukamilika mwaka 2017.

“Natambua kuwa Makao Makuu ya UNEP yapo Kenya, napendekeza na huku Tanzania muwe na Ofisi ili kuongeza kasi ya ufuatiaji na utekelewa miradi hii ambayo ni muhimu kwa ustawi wa kijamii na kiuchumi kwa wananchi wetu” alisema Dkt. Muyungi.

Naye Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la UNEP Kanda ya Afrika, Bi. Rose Mwebaza amepongeza jitihada zinazofanywa na Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais ya kukabiliana na uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi na kusisitiza kuwa Shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika Uhifadhi wa mazingira nchini.

Mkurugenzi huyo amesema suala la kukabiliana na tatizo la uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi sio la Serikali pekee hivyo ni muhimu kwa Serikali kushirikiana ipasavyo na mashirika yasiyo ya kiserikali katika kupambana na tatizo ili kupata suluhu ya kudumu.

Settings