UNEP: Mradi wa EBARR umeleta mafanikio makubwa kwa wananchi

Feb, 02 2024

Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) limetoa pongezi kwa usimamizi mzuri wa Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBARR) ambao umeleta mafanikio makubwa.

Pongezi hizo zimetolewa na Mwakilishi wa UNEP Tanzania, Bi. Clara Makenya wakati wa ziara ya ujumbe kutoka shirika hilo ulipofanya ziara ya kutembelea mradio huo katika Halmashauri ya Mpwapwa mkoani Dodoma.

Bi. Clara amesema hiyo ni hatua kubwa iliyofanywa na waratibu wa mradi huo ambao umekuwa wa mafanikio yaliyotarajiwa yanatimia kwa asilimia kubwa kwenye utekelezaji wake.

Katika ziara hiyo wamejionea shughuli mbalimbali wanazofanya wananchi waliowezeshwa na mradi ufugaji wa nyuki, visima, mashine ya kukamulia alizeti, majosho pamoja na kliniki ya mifugo.

“Tunaamini hata hivi vichache vilivyosalia katika utekelezaji utakamilika kwa wakati na kufanya kile kilichokusudiwa kwa wananchi wa kila eneo kunufaika na mradi hii,” alisema Bi. Clara.

Kwa upande wake Mratibu wa EBARR kitaifa, Dkt. Makuru Nyarobi aliwaomba wanakijiji kuendelea kutunza miradi hiyo ili iweze kukaa muda mrefu na kuzaa matunda.

“Wasimamizi wakubwa wa kila mahali ni nyie mliopo hapa ambao kila siku mnashughulika na kuwepo eneo la mradi, hivyo kikubwa ni kuwa makini katika usimamizi na kuendesha miradi hii,” alisema Dkt. Nyarobi.

Naye, Mratibu wa Wilaya ya Mpwapwa Bw. AzizBiru aliishukuru Ofisi ya Makamu wa Rais kwa namna walivyoisaidia jamii hasa Kata ya Mng’hambi kuondokewa na kero ya kufuata huduma umbali mrefu.

“Awali wananchi walikwenda mbali kukamua alizeti yao lakini baada ya Ofisi ya Makamu wa Rais kuweka mashine hapa wakulima wanafanya kazi kwa unafuu na muda mfupi, imeajiri vijana wengi na wengine kujiajiri chanzo ni miradi hii,” amsema Biiru.

Settings