Serikali imewataka wananchi na wadau katika mikoa ya Pwani na Lindi kuendelea kulinda maeneo tengefu na hifadhi ya bioanuai ili yaendelee kubaki na ubora na viwango vilivyoainishwa kitaifa na kimataifa.
Hayo yamesemwa wilayani Rufij mkoani Pwani na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis wakati alipokuwa akizindua hifadhi hai ya Rufiji- Mafia- Kibiti-Kilwa (RUMAKI).
Mhe. Khamis amesema mifumo ikolojia iliyopo katika Hifadhi Hai ni miongoni mwa bioanuai muhimu za Ukanda wa pwani ya Afrika Mashariki inayohifadhi bioanuai nyingi na za kipekee zinazotambulika kitaifa na kimataifa.
”Tunapaswa kufanya kila linalowezekana kuhakikisha kuwa Hifadhi Hai hii inabaki kuwa kwenye ubora na viwango vinavyokubalika kwa mujibu wa vigezo vyetu vya ndani na vya UNESCO (Shirika la Sayansi, Elimu na Utamaduni la Umoja wa Mataifa),” amesema Khamis.
Ameongeza kuwa Hifadhi Hai ya RUMAKI ni kielelezo kizuri cha juhudi nyingi zilizofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo mashirika ya kimataifa kwa miaka mingi ambayo inaenda sambamba na dhamira na malengo ya uhifadhi maeneo tengefu, hifadhi ya malikale na bioanuai.
Aidha Mhe. Khamis amelitaka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kushirikiana na taasisi mbalimbali za Serikali Kutayarisha mipango endelevu na shirikishi ya kulinda, kuhifadhi na kuendeleza hifadhi hiyo ili iendelee kubaki katika ubora wake.
Naibu Waziri Khamis amehimiza wananchi kujiepusha na uharibifu wa mazingira ikiwemouchomaji moto, ukataji misitu ikiwemo mikoko na uvuvi haramu na kuitaka NEMC kutumia mfumo maalum wa tahadhari za majanga ndani ya hifadhi hizo.
Amefafanua kuwa iwapo hifadhi hai ya RUMAKI itaendelea kulindwa na kuhifadhiwa kwa kuzingatia viwango na vigezo vya kitaifa na kimatifa itasaidia shughuli endelevu za kijamii, kiuchumi, kitalii na kimazingira na hivyo kubaki katika mtandao wa Hifadhi Hai Duniani.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tafiti za Mazingira wa NEMC, Dkt. Menan Jangu amewapongeza wananchi wa Wilaya za Rufiji, Mafia na Kilwa kwa kuendelea kutunza mazingira juhudi ambazo zimeweza maeneo hayo kutambulika kimataifa.
Amesema NEMC itaendelea kuratibu masuala ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira kupitia kwa wananchi na taasisi mbalimbali na kuanisha maeneo yote yenye sifa na vigezo vya kutambulika kimataifa.
”Tunapokuwa na eneo la hifadhi hai lina sifa na malengo makuu matatu ambayo ni maendeleo endelevu, uhifadhi na utunzaji wa viumbe hai vinavyotunzwa kwa faida ya vizazi vya sasa na baadae” amesema Dkt. Menan.
Naye Mwakilishi kutoka Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira Ulimwenguni (WWF), Bi. Joan Itanisa amesema ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Shirika hilo katika uendelezaji wa miradi ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira nchini.
Ameongeza kuwa uzinduzi wa hifadhi hiyo ni moja ya ahadi zilizowekwa na Wakuu wa Nchi mbalimbali duniani kuwa ifikapo mwaka 2030 asilimia 30 ya eneo la dunia iwe imehifadhiwa na kupongeza juhudi utayari wa Tanzania katika kutekeleza azimio hilo.
“Uzinduzi wa RUMAKI ni ishara kuwa Tanzania ipo mstari wa mbele katika kuwa kinara wa masuala ya uhifadhi...Tutaendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha wananchi wanaozunguza hifadhi hizi wanapata manufaa kutokana na uhifadhi huu” amesema Itanisa.