Serikali yaendelea kufungua milango uwekezaji wa biashara ya kaboni

Apr, 06 2024

Serikali imeendelea kufungua milango ya uwekezaji wa biashara ya kaboni pamoja na nishati safi, hatua itakayosaidia katika kuhakikisha hifadhi ya mazingira inakuwa endelevu.

Kupitia uwekezaji unaotarajia kufanyika hapa nchini katika biashara ya kaboni, takriban dola milioni 100 kila mwaka zinatarajiwa kupatikana na hivyo kukuza uchumi wa nchi.

Hayo yamebainika wakati wa kikao kati ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo na ujumbe kutoka Shirika la C-Quest Capital (CQC) ambao ni wadau wa mazingira.

Katika mazungumzo na Meneja Mkazi wa CQC Bw. Gabriel Mwalo aliyeambatana na ujumbe kutoka shirika hilo wamejadili miradi mbalimbali itakayochochea hifadhi ya misitu kwa kupunguza ukataji wa miti na kutunza ardhi.

Waziri Dkt. Jafo amepongeza shirika hilo kwa nia yake ya kuwekeza katika biashara ya kaboni ambapo amesema Serikali imewapa fursa ya kukutana na Kituo cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) cha Morogoro kwa ajili ya utekelezaji.

Halikadhalika, Waziri Jafo na shirika la CQC wamejadili mradi wa kuzalisha na kusambaza majiko sanifu 270,000 kwa mikoa nane nchini ambao utasaidia kupunguza ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa.

Amesema shirika hilo limeonesha dhamira ya kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhamasisha wananchi kutumia nishati safi ya kupikia hivyo itaendelea kuwaunga mkono ili kufikia azma ya kusitisha kabisa matumizi ya kuni na mkaa ili kunusuru misitu na afya ya binadamu.

Kwa upande wake Meneja Mkazi wa CQC Bw. Mwalo amesema dhamiira ya shirika hilo ni kuwekeza nchini katika maeneo ya vijijini katika nishati safi ya kupikia na mbinu bora za kilimo endelevu kitakachowawezesha wananchi kujiinua kiuchumi.

Kupitia hatua hiyo ameutambulisha kwa Waziri Jafo mradi wa kilimo endelevu ambacho kinatumia mimea kurutubisha ardhi badala ya kemikali.

Amesema kuwa mradi huo utakatekelezwa na shirika hilo nchini ambao uko katika hatua za usajili utasaidia kurutubisha na kuhifadhi ardhi bila kuathiri mazingira.

Ujumbe wa shirika hilo ulihusisha pia Afisa Mkuu wa Fedha Bw. Mark Woodwall, Meneja Mkuu wa Alliance Ginneriers Bw. Boaz Ogola na Mtaalamu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu.

Kwa upande wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Mkurugenzi wa Mazingira Bi. Kemilembe Mutasa, Mkurugenzi wa Sera na Mipango Bw. Ignas Chuwa, Mkurugenzi Msaidizi wa Mazingira Dkt. Paul Deogratius Paul walishirika kikao hicho.

Settings