Miaka 61 ya Muungano bila ya walioshiriki kuchanganya udongo

Feb, 26 2025

Ifikapo Aprili 26, 2025 Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakuwa inatimiza miaka 61 tangu kuasisiwa kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Aprili 26, 1964.

Tukio la kuchanganya udongo wa Tanganyika na Zanzibar lililofanywa na Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Aprili 26, 1965 ikiwa ni mwaka mmoja wa Muungano, lilihusisha vijana wane wa Kitanzania wawili kutoka Tanganyika na wawili kutoka Zanzibar.

Hata hivyo, ikiwa mwaka huu Muungano unapotimiza miaka 62 unaadhimishwa bila ya uwepo wa Watanzania hao wane ambao walishiriki tukio la kuchanganya udongo.

Miongoni mwa Watanzania hao ni Bi. Sifael Mushi ambaye alifariki Februari 20, 2025 jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu na amezikwa Februari 26, 2025 Machame wilayani Hai Mkoa wa Kilimanjaro.

Katika Ibada ya kumuombea Marehemu Sifael kwenye kwenye Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Nkwarungo kabla ya maziko nyumbani kwake, Serikali ilishiriki na kutoa salamu za pole.

Akitoa salamu za pole Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis alisema Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais inatambua na kuthamini mchango wa walioshiriki katika kuasisi na kuudumisha Muungano hususan wakati tukio la kuchanganya udongo wa Tanganyika na Zanzibar.

Naibu Waziri Khamis amemwelezea Bi. Sifael Mushi kuwa, alikuwa mzalendo ambaye hakusita wakati wote kueleza mazuri yote na faida za Muungano huu adhimu hususan kwa vijana ili kuulinda na kuutetea.

“Bi. Sifaeli alikuwa ni mmoja wa vijana walioshiriki tukio la kuchanganya udongo wa Tanganyika na Zanzibar lililofanyika tarehe 26 Aprili, 1965 katika sherehe za mwaka mmoja wa Muungano zilizofanyika katika Uwanja wa Uhuru, Jijini Dar es Salaam.

Alishiriki katika tukio hilo akiwa kijana mwenye umri wa miaka 32 pamoja na wenzake watatu (Mzee Hassan Omari Mzee kutoka Zanzibar, Bi. Khadija Abasi Rashid kutoka Zanzibar na Bw. Hasanieli Elisaeli Mrema kutoka Tanzania Bara),“ amesema Naibu Waziri. Amesema kwa kutambua mchango huo, Ofisi ya Makamu wa Rais pia iliwahi kuwaalika wazee hao Bungeni wakati wa kusoma hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais tarehe 3 Mei, 2016 na walishiriki ambapo tukio la mwisho ambalo alishiriki na wenzake watatu ni Maadhimisho ya miaka 54 ya Muungano katika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma tarehe 26 Aprili, 2018, tukio hili aliweza kushiriki na wenzake wote watatu.

Pia, Mhe. Khamis alisema Serikali inatambua mchango mkubwa wa wazee hao wanne ambao wote ni marehemu, hivyo mwaka 2014 walitunukiwa Nishani ya Kumbukumbu ya Miaka 50 ya Muungano Daraja la Nne. Nishani hizi zilitolewa na Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano, Awamu ya Nne katika Hafla iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam tarehe 26 Aprili, 2014.

Aidha, Naibu Waziri aliwasilisha salamu za pole kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na salamu kutoka wa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango.

Akitoa salamu zake Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini ya KKKT Frederick Shoo ambaye aliongoza ibada ya kumuaga Marehemu Sifael aliwataka Watanzania kuwekeza katika elimu.

Alisema ni muhimu kuiga mazuri ya marehemu hususan katika suala la elimu ambalo aliitumikia kwa moyo wote katika kipindi cha uhai wake wakati anafundisha wanafunzi.

Mara baada ya ibada hiyo mwili wa Marehemu ulipelelekwa nyumbani kwake kwa ajili ya maziko ambayo yalihudhuriwa na ndugu, jamaa na wananchi mbalimbali.

Settings