‘Serikali kuendelea kulinda watoto dhidi ya mabadiliko ya tabianchi’

Nov, 22 2023

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema Tanzania itaendelea kuwalinda watoto dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

Amesema hayo wakati akihutubia kwenye Maadhimisho ya Siku ya Mtoto Duniani leo Novemba 22, 2023 jijini Arusha ambapo amesisitiza Serikali kuendelea kuwa imara katika kuwaepusha na athari hizo.

Dkt. Jafo amesema kuwa watoto wamekuwa waathirika wakubwa wa athari za mabadiliko ya tabianchi hapa nchini na duniani kwa ujumla ikiwemo mafuriko na ukame ambao husababisha baa la njaa.

“Ndugu zangu viongozi Naomba niwathibitishie kuwa dhamira ya Serikali ya Tanzania ni kuwalinda watoto dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi", amesema Waziri Jafo.

Amewataka wataalamu wa mazingira kujikita katika kumjengea mtoto uwezo wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwani chakula kinapokosekana kundi hilo ndilo huathirika zaidi.

Ameongeza kuwa maadhimisho haya yaliyotokana na mkataba wa kimataifa wa Haki za mtoto ya mwaka 1989,ambapo nchi ya Tanzania iliridhia kulindwa kwa za haki watoto sambamba na kuwasaidia namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Akimkaribisha Waziri Jafo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu Bw. Amon Mpanju amesisitiza sala la kulindwa kwa haki za watoto na namna ya kukabikiana na mabadiliko ya tabianchi.

Amesema kaulimbiu hiyo ni dhahiri imekuja kwa wakati muafaka kwa ajili ya kuwasaidia watoto kutambua na kuwapatia elimu ya kutosha ili wawe mabalozi wazuri wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Mpanju ameongeza kuwa Serikali inaratibu na kusimamia haki zote za watoto ikiwemo haki ya kuishi na kumlinda didhi ya vitendo vyote vya ukatili.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Watoto (UNICEF) nchini Bi. Elke Wisch amepongeza juhudi za Tanzania katika kupigania na kuziendeleza haki za watoto.

Settings