Serikali kubainisha maeneo ya kuboreshewa mazingira ya kukabili mabadiliko ya tabianchi

Jan, 31 2024

Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na wizara za kisekta imeanza kufanya tathmini nchi nzima kubainisha maeneo yanayohitaji kufanyiwa maboresho kukabiliana na athari za kimazingira.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Mtambwe Mhe. Khalifa Mohammed Issa aliyetaka kujua lini Serikali itafanya utafiti kuyabaini maeneo yaliyoathiriwa na mabadiliko ya tabianchi.

Katika kushughulikia changamoto ya mabadiliko ya tabianchi Dkt. Jafo amesema kuwa Serikali imeanza kuyafanyia kazi maeneo hayo kwa kutekeleza miradi ya mazingira pande zote mbili za Muungano.

Amesema kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais inaendelea na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa tuta linalozuia maji ya bahari kuingia kwenye makazi na mashamba unaotekelezwa eneo la eneo la Sipwese Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini, Pemba.

Halikadhalika, amesema mradi huo unatekelezwa pia katika eneo la Mikindani, Mtwara ambako kunajengwa ukuta utakaosaidia kupunguza kasi ya maji ya bahari kuingia kwenye makazi ya watu na kuta kwa ajili ya kurejesha fukwe katika hali yake.

“Katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imetuma timu ya wataalamu ikishirikiana na wizara za kisekta kufanya tathmini ambayo itatusaidia kubaini maeneo gani yenye changamoto na kuyafanyia kazi hivyo kuhakikisha nchi yetu inakuwa salama,” amesisitiza Waziri Dkt. Jafo.

Awali, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamisalisema Serikali inaendelea na kampeni za kuhamasisha wananchi kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ikiwemo zoezi la upandaji wa miti katika maeneo yote nchini.

Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu Mhe. Mariam Nasoro Kisangi aliyeuliza mkakati ya Serikali wa kupambana na mabadiliko ya tabianchi, Mhe. Khamis alisema Ofisi ya Makamu wa Rais inafanya kampeni hizo kwa kushirikiana na taasisi kuhamasisha ubunifu, utafiti na uendelezaji wa teknolojia za kukabiliana na changamoto hiyo.

Mhe. Khamis alibainisha kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeandaa na kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (2021-2026) na Mpango Kabambe wa Taifa wa Hifadhi ya Mazingira (2022-2032).

Aidha, alisema kuwa kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar upo Mkakati wa Mabadiliko ya Tabianchi Zanzibar (2014-2030) ambao unatekelezwa kupitia Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais yenye dhamani ya mazingira.

Alisema Serikali inayo Mipango ambayo kwa pamoja imeelezea changamoto na hatua mbalimbali za kuzifuata katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi yanayoathiri maeneo mbalimbali hapa nchini.

“Tunatambua mkakati tulionao wa kusafisha mito na tayari Mhesehimiwa Waziri (Dkt. Jafo) alishaunda Kamati na kubaini chanzo mkusanyiko wa mchanga mkoani Dar es Salaam na kuziba mifereji nasi tunaendelea kutoa elimu na kusimamia Sheria ya Mita 60 na Usafishaji wa mito kwa kutoa mchanga na takataka nyingine,” alisema Mhe. Khamis.

Settings