Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali itaendelea kuchukua hatua madhubuti kutatua changamoto za Muungano kila zinapojitokeza.
Mhe. Dkt. Samia amesema hayo wakati wa kufungua rasmi Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma leo tarehe 14 Novemba, 2025.
Amesema kuwa tunapozungumzia umoja wa kitaifa tunaongozwa na uwepo wa Tunu ya Muungano hivyo, kuudumisha kuimarisha na kuuenzi Muungano kutaendelea kuwa kipaumbele cha Serikali.
Wakati hayo yakijiri tayari Serikali kati ya mwaka 2021 hadi 2025 imeshazipatia ufumbuzi hoja 15 za Muungano hivyo, kuendelea kuleta amani, umoja na mshikamano miongoni mwa Watanzania.
Akiendelea kuhutubia Bunge, katika hatua nyingine Rais Mhe. Dkt. Samia amesema kuwa Serikali italipa kipaumbele suala la maendeleo ya uchumi wa buluu.
Sekta ya Uchumi pamoja na mambo mbalimbali inajumuisha shughuli za uvuvi, ikiwemo kilimo cha kisasa cha mazao ya baharini na mabwawa.
Aidha, Mhe. Rais Dkt. Samia amebainisha kuwa itaendeleza utekelezaji wa Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia ambao una lengo la kufikia asilimia 80 ya Watanzania wanaotumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034, hatua itakayopunguza uharibifu wa mazingira na kulinda afya za watumiaji.
Halikadhalika, amesema utunzaji wa mazingira ni suala muhimu katika maendeleo yanayopangwa na kuyatarajia hivyo, kuelekea mwaka 2030, Serikali itaimarisha usimamizi wa biashara ya kaboni kwa manufaa ya wananchi wa maeneo husika na taifa kwa ujumla.
Amefafanua kuwa hatua hiyo itasaidia katika kupunguza migogoro ya mikataba inayoingiwa kupitia biashara ya kaboni katika siku za usoni.