Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Prof. Peter Msoffe amesema ushiriki wa Tanzania katika mikutano ya Mabadiliko ya Tabianchi kumekuwa na fursa mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa fedha za miradi na kujengea uwezo wataalamu wetu.
Prof. Msoffe ameyazungumza hayo wakati akifungua kikao cha kwanza cha Kamati ya Kitaifa ya Maandalizi ya Mkutano wa 30 wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP30) kilichofanyika Dodoma, Agosti 25, 2025.
“Lengo kuu la kikao hiki ni kufanya maandalizi ya ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa COP30 kwa kujadiliana na kufikia maazimio ya namna tutakavyoshirikiana kufanikisha ushiriki wa Nchi yetu katika Mkutano huo.”
“Uwepo wenu hapa unaonesha moyo wenu wa dhati wa kuyatetea mazingira ya nchi yetu na dunia kwa ujumla kwa ajili ya vizazi vya sasa na vya baadaye” amesema Prof. Msoffe.
Ameongeza kuwa kikao hicho kina jukumu la kuandaa Mpango-kazi na kugawana majukumu miongoni mwa wataalam ili kuwezesha utekelezaji wa shughuli za maandalizi za COP30.
Amesema Ofisi ya Makamu wa Rais ndio mratibu na msimamizi wa utekelezaji wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC). Kwa kuzingatia Majukumu hayo, OMR imeandaa kikao hicho kwa ajili ya kuwa na maandalizi ya pamoja miongoni mwa Wizara, Idara, na Taasisi za Serikali.
“Kwa kushiriki Kikao hiki mnatarajiwa kuangazia zaidi maboresho ya Mapendekezo ya Ushiriki wa Wizara na Taasisi katika Mkutano wa COP30 kwa kufanya uchambuzi zaidi ili kupata mwelekeo wa maandalizi ya pamoja.”
Mkutano wa COP30 utafanyika katika Jiji la Belem, Brazil kuanzia tarehe 10 hadi 21 Novemba, 2025 ambapo Ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unatarajiwa kuongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.