Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Kemilembe Mutasa amesisitiza umuhimu wa kuhifadhi mazingira ya ardhi oevu kutokana na umuhimu wake katika kutoa mahitaji muhimu kwa wanadamu na viumbe wengine.
Amesema hayo wakati akifungua mkutano wa Viongozi wa Mazingira wa kujadili jinsi ya kulinda ardhioevu ya Afrika Mashariki kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandishi Cyprian Luhemeja jijini Dar es Salaam.
Bi. Mutasa ametahadharisha kuhusu kupungua kwa ardhi oevu kutokana na upotevu wa makazi, uchafuzi wa mazingira, mabadiliko ya hali ya hewa, matumizi ya ardhi oevu yasiyo endelevu. Amesema kubadilishwa kwa ardhi oevu kwa ajili ya kilimo, kupanuka kwa miji, ujenzi wa miundombinu kunaharibu mifumoikolojia.
Amesisitiza umuhimu wa kuwepo kwa mipango kamilifu ya matumizi ya ardhi ili kulinda mifumo ikolojia hii muhimu akisema upotevu wa makazi bado ni tishio kubwa na ardhioevu kubadilishwa kwa upanuzi wa kilimo, ukuaji wa miji na maendeleo ya miundombinu.
Pia, Bi. Mutasa amehimiza juhudi za pamoja katika kutunga sera madhubuti za mipango ya matumizi ya ardhi zinazotoa kipaumbele katika hifadhi ya maeneo oevu na maendeleo endelevu.
Ameongeza kuwa uchafuzi ni tatizo lingine kubwa, ambapo taka za viwandani, majitaka ya kilimo, na taka za nyumbani yanachafua maeneo oevu. Uchafuzi huu unasababisha upotezaji wa bayoanuai na uharibifu wa mazingira kwa ujumla.
Mkurugenzi huyo amehimiza usimamizi bora wa taka, utekelezaji wa sheria za mazingira, na uwekezaji katika miundombinu ya maji taka ili kukabiliana na changamoto hii.
Pia, amehimiza kuunganishwa kwa mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika mipango ya usimamizi wa ardhioevu, ikiwa ni pamoja na kurejesha ardhioevu iliyoharibiwa, utekelezaji wa hatua za kuhifadhi maji, na uhamasishaji wa suluhisho zinazotegemea asili.
Amesisitiza haja ya kuoanishwa kwa sera, na ushirikiano madhubuti na jumuiya za kiraia, sekta binafsi na watafiti na wanataluma. Matumizi yasiyo endelevu ya rasilimali za ardhioevu ni suala lingine linalotishia maeneo ya ardhi oevu, ambapo uvunaji kupita kiasi wa mimea ya majini, uvuvi wa kupita kiasi, na matumizi ya maji yasiyoendelevu unamaliza rasilimali hizi.
Mkutano wa Baraza la Uongozi la RAMCEA, ambacho ni kituo cha kikanda chini ya Mkataba wa Ramsar kuhusu Ardhioevu, uliwaleta pamoja wawakilishi kutoka Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, na Sudan Kusini katika ngazi ya makatibu wakuu wa wakuu wa taasisi zinazosimamia masuala ya hifadhi ya arfdho oevu.
Washiriki wengine wa mkutano huo walikuwa wawakilishi wa mshairika ya kimataifa yanayohusika na hifadhi ya ardhi oevu. Mkutano huo ulilenga kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kuandaa mipango ya kulinda mifumo ikolojia ya ardho oevu.
Mkutano huo ulitanguliwa na ziara ya siku moja kutembela maeneo ya ardhi oevu katika Kijiji cha Nyamisati katika Wilaya ya Kibiti Mkoa wa Pwani ambapo wajumbe wa mkutano walijionea shughuli za uhifadhi wa maeneo oevu katika eneo hilo maarufu kwa misitu ya mikoko.
Wataalamu wa mazingira na watunga sera kutoka Afrika Mashariki na mashirika ya kimataifa walikutana jijini Dar es Salaam wiki hii kwa ajili ya mkutano muhimu wa Baraza la Uongozi la Kituo cha Ramsar cha Afrika Mashariki (RAMCEA) kujadili masuala mbalimbali yanayohusu usimamizi wa maeneo ya ardhi oevu katika nchi za Afrika Mashariki.