Ofisi ya Makamu wa Rais yawasilisha taarifa ya bajeti kwa Kamati ya Bunge

Mar, 20 2024

Ofisi ya Makamu wa Rais itashiriki katika Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2024 ili kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kuhusu ya umuhimu wa kuhifadhi mazingira.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema alipowasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka wa fedha 2023/24 na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2024/25 kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira jijini Dodoma leo Machi 20, 2024.

Amesema kuwa hatua hiyo itasaidia kuwajengea wananchi uwezo wa kushiriki katika zoezi la upandaji wa miti, usafi wa mazingira na shughuli nzima za utunzaji wa mazingira kwa ujumla.

Mbio za Mwenge wa Uhuru 2024 wenye kaulimbiu ‘Tunza Mazingira na Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Ujenzi wa Taifa Endelevu zinatarajiwa kuzinduliwa April 02, 2024 mkoani Kilimanjaro.

Pamoja na mambo mbalimbali, katika taarifa aliyowasilisha, Dkt. Jafo amesema Ofisi ya Makamu wa Rais inatarajia kuendelea kusimamia, Kuratibu na Kufuatilia Utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 2021.

Amesema kuwa katika hatua hiyo pia Mkakati wa utekelezaji na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, Sura 191 katika Sekta na Mamlaka za Serikali za Mitaa unatarajiwa kukamilika.

Dkt. Jafo amesema Ofisi pia itakamilisha mapitio ya Sheria Usimamizi wa Mazingira, Sura 191; 32 pamoja na Taarifa ya Nne ya Hali ya Mazingira Nchini.

Aidha, mifumo ya usimamizi wa utekelezaji wa Sheria ya Mazingira, Sura 191 kupitia Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira pamoja na Mamlaka za Serikali za Mitaa itakamilishwa.

Shughuli nyingine ni kuandaa Kanuni ya Haki ya kulipwa fidia kutokana na uharibifu wa Mazingira, Kanuni ya Usimamizi Jumuishi ya Mazingira ya Ukanda wa Bahari pamoja na kuendelea uratibu utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (2022 - 2032).

Settings