Ofisi ya Makamu wa Rais yawanoa washiriki COP28

Oct, 25 2023

Ofisi ya Makamu wa Rais imeendesha Warsha ya Wadau wa Kitaifa kuhusu maandalizi ya ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa 28 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi COP28.

Warsha hiyo imefanyika jijini Arusha Oktoba 24, 2023 kwa lengo la kujenga uelewa kwa washiriki kuhusu fursa mbalimbali za fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zinazotolewa na Mifuko ya Kimataifa na nchi mbalimbali duniani.

Akifungua warsha hiyo Kaimu Mkurugenzi wa Mazingira, Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Paul Deogratias amesema ni fursa kwa washiriki kujadili na kutoa maoni kuhusu msimamo wa nchi katika Mkutano wa COP28 unaotarajiwa kufanyika Dubai, Muungano wa Falme kuanzia Novemba 30 hadi Desemba 12, 2023.

Amesema warsha hiyo inahusisha mawasilisho na mijadala ya ajenda mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupitia yaliyojiri katika Mkutano wa COP27, mafanikio, changamoto na mpango mkakati kuelekea COP28, kufanya uchambuzi wa kina kuhusu mada zitakazowasilishwa pamoja na kujadili kuhusu msimamo wa nchi.

“Tunatarajia kuwa na Warsha ya Kitaifa ya Wadau itakayofanyika Oktoba 26, 2023 ambayo itahusisha viongozi, wataalamu na wadau wengine walioalikwa kutoka katika Wizara, Mashirika ya Umma, Mashirika ya Maendeleo, Sekta Binafsi na Mashirika ya Kiraia,” amesema.

Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa COP28 utaongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ukihusisha viongozi na watalaamu kutoka Wizara za Kisekta, Idara za Serikali, Mashirika ya Umma, Vyuo Vikuu, Sekta binafsi, Asasi za Kiraia, Vijana na Wanahabari.

Kaulimbiu ya kitaifa ni: “Kuimarisha Kilimo Himilivu na Uchumi wa Bluu katika Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi” ikitoa msisitizo katika matumizi ya teknolojia na mbinu bora zinazozingatia changamoto za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Pia, kaulimbiu hii inalenga kujenga uwezo wa kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi katika kukuza uchumi wa buluu na kuchochea maendeleo endelevu.

Settings