Naibu Waziri wa Maliasili atembelea banda la Tanzania COP29

Nov, 20 2024

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dunstan Kitandula ametoa wito kwa washiriki wote wa COP29 kutoka Tanzania kutumia fursa ya ushiriki wao katika kuendelea kuitangaza nchi kimataifa.

Ametoa wito huo alipotembelea banda la maonesho la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katikaMkutano wa 29 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP29) unaoendelea jijini Baku, Azerbaijan, leo Novemba 20, 2024.

Mhe. Kitandula amewapongeza viongozi na washiriki wote kwa ujumla kwa umoja wao na hatimaye kufanikisha ushiriki kwenye mkutano huo mkubwa unaozikutanisha nchi mbalimbali duniani.

Amewapongeza kwa kuandaa banda la maonesho ambalo limekuwa kivutio kwa wadau kutoka mataifa mbalimbali kwa kuwa na taarifa mbalimbali kuhusu hifadhi ya mazingira katika sekta mbalimbali nchini Tanzania.

“Tumeziona kazi mnazofanya hongereni sana, mmetuwakilisha vizuri na tunategemea haya yote mliyoyafanya tuyapate kwenye taarifa na mtushauri nini cha kufanya ili tusonge mbele, isiwe tu mmeshiriki halafu basi,“ amesisitiza.

Aidha, Naibu Waziri Kitandula amewasihi washiriki hao kuiga mazuri yote waliyoyashuhudia na kujipanga kufanya vizuri zaidi katika mkutano ujao wa COP30 unaotarajiwa kufanyika nchini Brazil mwaka 2025.

Amesema kufanya vizuri kwa washiriki wa Tanzania katika mkutano wa COP29 ndio kuifanya nchi ionekane na kuwavutia watalii wengi zaidi kufika na si tu kuzuru vivutio bali pia kuwekeza katika miradi ikiwemo ya mazingira.

Halikadhalika, Naibu Waziri Kitandula amesema amefarijika kuona kazi kubwa imefanyika katika sekta misitu na nishati safi ya kupikia ambayo ni ajenda kubwa inayochagizwa nchini Tanzania kwa lengo la kupunguza ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa.

Pia, amesema kwa vile suala la utalii kwa mara ya kwanza limejumuishwa katika mkutan huu hiyo imekuwa ni chachu sasa ya kupata uzoefu na kujipanga vizuri zaidi ili kuhamasisha utalii.

Settings