NAIBU WAZIRI KHAMIS: PANDENI MITI KUTUNZA MAZINGIRA

Jul, 17 2024

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis amewahimiza Watanzania kuwa na utamaduni wa kupanda miti ili kutunza mazingira.

Ametoa wito huo wakati wa zoezi la upandaji wa miti lililoandaliwa na Shule ya Msingi ya Wasichana Mkuza wilayani Kibaha mkoani Pwani ikiwa ni sehemu ya kumbukizi ya siku ya kuzaliwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango.

Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Waziri Khamis amesema kuwa ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha anashiriki kikamilifu katika hifadhi na utunzaji wa mazingira.

Mhe. Khams amesema kuwa katika suala la utunzaji wa mazingira jamii inapaswa kushiriki kikamilifu katika zoezi la upandaji wa miti hasa ya matunda na vivuli ili kukijanisha nchi na kupunguza uharibifu wa mazingira.

“Niwaombe ndugu zangu hapa tunakumbuka kuzaliwa kwa Mheshimiwa Makamu wa Rais kwa kufanya zoezi la kupanda miti, nasi wananchi tuwe na utamaduni wa kupanda miti tunasherehekea siku zetu za kuzaliwa na matukio mengine,” amesema.

Aidha, Mhe. Khamis amesema kuwa Serikali ilianzisha kampeni ya ‘Soma na Mti‘ kwa wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo ili kuongeza wigo wa upandaji wa miti na matokeo yake ni kusaidia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Halikadhalika, amewaomba Watanzania kuendeleza matumizi ya nishati safi kwa ajili ya kupikia na kuachana na matumizi ya kuni na mkaa ambayo huchangia ukataji wa miti.

Tayari Serikali imeandaa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ambao unatoa mwelekeo wa nchi wa kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa lengo la kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati hiyo ifipako mwaka 2034.

Sanjari na hilo, pia Naibu Waziri Khamis ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi watunze vyanzo vya maji ili viwaletee manufaa katika vizazi vya sasa na vijavyo.

Kwa upande wake Msaidizi wa Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani Chediel Lwiza amesema zoezi la upandaji wa miti ni kuunga mkono Serikali kuhakikisha hifadhi ya mazingira inakuwa endelevu.

Amesema utunzaji wa mazingira ni ishara ya kutambua uumbaji wa Mungu hivyo kama mwanadamu ataharibu mazingira atakuwa anaenda kinyume na uumbaji wa Mungu.

Settings