Naibu Katibu Mkuu Nyamanga afungua mafunzo kwa wasimamizi wa miradi

Jan, 25 2022

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais- Mazingira Bw. Edward Gerald Nyamanga kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano na Mazingira amefungua mafunzo ya Usimamizi wa miradi kwa Watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais leo Januari 25, 2022 mkoani Morogoro.

Mafunzo hayo yanatolewa na Taasisi ya Usimamizi wa Miradi Tanzania (TIPM), yenye lengo la kuwajengea uwezo katika usimamizi mzuri wa miradi ili kujua misingi muhimu ya kuwezesha miradi kufikia malengo yanayotarajiwa na serikali pamoja na jamii kwa ujumla.

Aidha, Naibu Katibu Mkuu Mazingira Bw. Nyamanga ameeleza umuhimu wa mafunzo hayo kuwa yatawezesha Waratibu na Wataalamu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais kupata uelewa kuhusu Mpango Mkakati, taratibu zinazotumika kusimamia miradi, mpango wa majukumu, ufuatiliaji na utekelezaji unaohusisha wadau mbalimbali katika kusimamia nakutekeleza miradi nakuleta tija kwa maendeleo ya taifa letu.

Amesema kuwa mafunzo haya yatawasaidia washiriki katika kuandaa mipango na bajeti pamoja na utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika miradi inayotekelezwa pamoja na kupata ujuzi wa kubuni miradi inayoweza kuwanufaisha wananchi kwa ujumla.

Mafunzo hayo ya siku 5 yanahusisha washiriki kutoka Idara na vitengo mbalimbali katika Ofisi ya Makamu wa Rais

Settings