Mradi wa LoCAL ni wa mfano

Nov, 02 2023

Mradi wa Uhimili na Kukabiliana na Athari za Mabadiliko ya Tabianchi (LoCAL) unaotekelezwa katika halmashauri za wilaya za Kondoa, Mpwapwa na Chamwino mkoani Dodoma umekuwa wa mfano kwasababu umeleta matunda mazuri.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Msaidizi Sera na Mipango kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Paul Laizer wakati wa Semina ya wadau ya kutathimini mabadiliko ya tabianchi kutokana na fedha za ndani na nje zilizotengwa katika bajeti ya Serikali kuanzia mwaka 2020 hadi 2023 iliyofanyika jijini Dodoma leo.

Laizer ametoa rai kwa washiriki wa semina hiyo kuzitendea haki fursa za namna hiyo zinapopatikana hii ili kuendelea kuaminiwa na washirika wa maendeleo kwani kwani tulianza kidogo na sasa tumepiga hatua ambayo hii ni ishara kwamba tunafanya vizuri.

Amesema fedha nyingi zinazotengwa kwenye miradi ya mazingira hazitumiki hivyo amesisitiza zifanye kazi hiyo na si vinginevyo na kwa muda uliopangwa.

“Niwashukuru wote, kwani kupitia mradi wa LoCAL kama nchi tunahitaji miradi mingi kama hii na tumeanza na Halmashauri tatu, hivyo ukitumika kama mfano kwa kufanya vizuri unawapa fursa wengine ya kuweza kufikiwa.”

“Tunalalamika miradi mingi haiendi sababu haina fedha lakini fedha zikija hazifanyi kazi ipasavyo, tunaleta fedha kwa ajili ya visima lakini havichimbwi, hivyo kuna changamoto katika usimamizi wa hii miradi fedha zinakuja na zinaletwa huko lakini halmashauri zinachelewa kutumika,” amesema Laizer.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Dk. Deogratius Paul Nyangu amehimiza ukweli na kasi katika utendaji kazi kwani kila wanapokutana na wadau moja ya vitu wanavyozungumza ni utunzaji wa mazingira.

Mratibu wa LoCAL- UNCDF Tanzania amesema walianza kwa kutokuwa na uhakika lakini mwisho wa siku walitumia changamoto zilizojitokeza kujifunza na hatimaye wamefanikiwa kupiga hatua na sasa matunda yanaonekana katika miradi waliyoifanya.

Settings