Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhandisi Hamad Yussuf Masauni amesema Serikali inaendelea na uchunguzi wa kimaabara kwa kufanya utafiti wa kuwabaini wadudu ili kuangamiza mmea wa gugumaji.
Akizungumza wakati alipotembelea eneo la Kigongo - Busisi mkoani Mwanza eneo ambalo limeathirika na gugumaji na serikali kuchukua hatua za haraka kukabilia na tatizo hilo ambapo hadi sasa zaidi ya tani elfu kumi za mmea huo zimeondolewa, amesema utafiti wa kimaabara utakuwa tayari yatakuwa mafanikio makubwa.
Amesema uchunguzi huo unaofanyika kwenye maabara iliyoko Kibaha mkoani Pwani baada ya ziara ya wataalam kwenda nchini Uganda ambao walijifunza namna ya kukabiliana na mmea wa gugumaji na kupitia ziara hiyo waligundua namna ambavyo Uganda walivyofanikiwa.
Ameongeza kuwa uchunguzi huo ni muhimu kwa sababu utawezesha kutumia njia ya kitaalam kuangamiza mmea wa gugumaji na kuepusha athari zingine kujitokeza sio katika eneo la Ziwa Viktoria pekee bali nchi nzima.
“Napenda nichukue fursa hii kumpongeza kwa dhati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kuchukua hatua kupitia maelekezo aliyoyatoa kwa Waziri Mkuu ambaye aliunganisha sekta zote husika ikiwemo Ofisi ya Makamu wa Rais.
“Ilitengenezwa timu ya pamoja ya wataalam ambayo imeweza kushauri na kwa pamoja tukaweza kushirikiana na viongozi wa wilaya na mkoa na hatimaye leo tumeona changamoto ya gugumaji limepungua kwa kiwango kikubwa,” amesema Waziri Masauni.
Ameongeza kuwa miongoni mwa fedha zilizotolewa na serikali kwa ajili ya zoezi hilo zinatumika kununua mitambo mahsusi kwa ajili ya shughuli za kuondoa gugumaji wakati wowote litakapojitokeza kwenye eneo hilo pamoja na maeneo mengine.
‘’Badala ya kuazima mitambo ambayo tulitumia fedha kwa ajili ya kuweka mafuta na huduma mbalimbali, sasa Serikali iko kwenye hatua ya mwisho ya ununuzi wa mitambo maalum kwa ajili ya shughuli hii.” Alisema Waziri Masauni.
Naye Mkuu wa Wilaya Sengerema mkoani Mwanza Mhe. Senyi Ngaga ameishukuru Serikali Kuu kwa kuchukua hatua za haraka za kukabiliana na mmea wa gugumaji kwenye eneo hilo ambapo shughuli za usafirishaji zilikuwa zikiathirika zaidi.
Mhe. Ngaga ameiomba Serikali kuharakisha mchakato wa ununuzi wa mitambo ya kisasa ya kuondoa mmea wa gugumaji ili kuepusha athari zaidi zinazoweza kujitokeza kwenye sekta ya usafiri, uvuvi na utalii.
Hata hivyo Meneja wa Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Jerome Kayombo amesema Ziwa Victoria kwa upande wa Tanzania limeathirika na magugumaji yaliyogawanyika katika makundi matatu ambayo ni Salvinia molesta, water hyacinth na gugumaji la asili.
“Uzalishaji wa wadudu unaoendelea katika maabara tutapofanikiwa kupata matokeo chanya wananchi watafundishwa jinsi ya kuwazalisha kwenye maeneo yao ya ziwa kisha kupandikiza kwenye maeneo yaliyoathirika”