Mhandisi Luhemeja: Ushirikiano wa Tanzania, Japan waimarika

Sep, 16 2025

Ushirikiano wa Tanzania na Japan umezidi kuimarika baada ya kuzinduliwa kwa Kamati ya Pamoja ambayo itasaidi katika Biashara ya Kabon hususani katika upatikanaji wa soko.

Kamati hiyo imezinduliwa leo Septemba 16, 2025 jijini Dar es Salaam ambapo Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema pamoja na kuzindua Kamati ya Pamoja lakini wamepitia kanuni na taratibu ambazo zitawaongoza.

Amesema Kamati hiyo pia inalenga kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Japan katika kushughulikia mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuendeleza miradi yenye tija kwa taifa.

Ameongeza kuwa kamati hiyo itarahisisha uratibu na ushauri wa kitaalamu, sambamba na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje katika sekta za nishati safi, kilimo endelevu na uhifadhi wa mazingira.

“Mwezi wa tano mwaka huu kule Japan, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mha. Yussuf Masauni alisaini mkataba wa mashirikiano kati ya Tanzania na Japan katika biashara ya Kaboni sababu wao wameanzisha taasisi ambazo zinakuja Afrika kutafuta miradi.

“Baada ya ule mkataba wa ushirikiano tukatengeneza Kamati ya Pamoja baina ya nchi hizi mbili ambapo leo (Septemba 16, 2025) ndio tumeizindua kamati, kanuni na taratibu za kuzifuata ikiwa pamoja na kuitambulisha miradi mbalimbali.” Amesema Mha. Luhemeja.

Ameongeza katika kupambana na mabadiliko ya Tabianchi kila nchi imepewa jukumu lake ambapo Japan imejiwekea malengo ya kupunguza hewa ukaa kwa 60% na sababu nchi hiyo imepiga hatua, hivyo inatafuta nchi washirika ili kushirikiana katika miradi mbalimbali ikiwemo usafirishaji, nishati safi na Uchukuzi.

Mha. Luhemeja amesema ushirikiano huo utasaidia Tanzania katika eneo la soko kutokana na mawazo mbalimbali yanayotokana na wadau kutoka nje ya nchi wanaokuja kuwekeza nchini katika eneo hilo na kufanya Taifa kuongeza kipato.

Kwa upande wake, Kaimu Balozi wa Japan nchini Tanzania, Mhe. Ueda Shoichi, amesema ushirikiano huo ni kielelezo cha dhamira ya Japan kushirikiana na Tanzania katika biashara ya kaboni, teknolojia, uwekezaji na maendeleo endelevu, hatua inayotarajiwa kuimarisha zaidi uhusiano wa kiuchumi na kijamii kati ya nchi hizo mbili.

Ameongeza huu ni mwanzo ambao utafungua zaidi fursa katika uwekezaji kwenye Biashara ya Kaboni na Japan ipo tayari kuwekeza baada ya kupata ushirikiano mzuri kutoka Tanzania.

Settings