Mamalishe Muheza wahamasishwa kutumia nishati safi ya kupikia

Apr, 15 2024

Mamalishe wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza mkoani Tanga wamehamasishwa kutumia nishati safi ya kupikia kwa kupewa mitungi 200 ya gesi na kuacha kutumia kuni na mkaa katika juhudi za kutunza na kulinda mazingira.

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Hamisi Mwinjuma akizungumza wakati wa Mbio za Mwenge Kitaifa 2024 wilayani humo Aprili 15, 2024 amesema kila mmoja anatakiwa kuwa mlinzi wa mazingira.

Mhe. Mwinjuma ambaye pia Mbunge wa Jimbo la Muheza mkoani ameongeza kuwa Mamalishe wanapotumia Nishati Safi sio tu wanalinda na kutunza mazingira lakini hata afya zao zinalindwa kwa kuwa matumizi ya mkaa na kuni huhatarisha afya za binadamu kwa njia moja au nyingine.

Kwa upande wake kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2024 Bw. Godfrey Mnzava amesema serikali inaendelea kutoa wito kwa jamii kutumia nishati safi na kuachana na kuni na mkaa sababu ya kulinda mazingira.

“Tumeanza kuhama huko katika matumizi ya mkaa na kuni na sasa tunatumia nishati mbadala hivyo viongozi tuzidi kutoa elimu na kuihamashisha jamii katika kutumia Nishati Safi,” amesema Bw. Mnzava.

Aidha, Afisa Maliasili na Mazingira Halmashauri ya Wilaya ya Muheza Bw. Cyprian Mselemu amesema katika kutunza mazingira halmashauri imetoa elimu kwa wananchi wa kijiji cha Kigombe kilichopo katika pwani ya Bahari ya Hindi kuacha kufanya shughuli za kibinadamu katika maeneo tengefu.

“Wavuvi walielimishwa juu ya zana bora za uvuvi ikiwa Pamoja na kufanya doria za mara kwa mara ili kuimarisha usimamizi bora wa rasilimali za bahari na kuwa na uvuvi endelevu wenye suluhisho la uhakika wa chakula, maisha na ustawi kwa jamii wenyeji na wilaya kwa ujumla.

“Halmashauri inafanya uhamasishaji kwa wananchi kutumia mbinu za asili za kuhifadhi vyanzo vya maji kama upandaji wa ngugu, mafukutu na matambazi kandokando ya vyanzo vya maji ambayo hutumika kama chujio la kuchuja takataka na uchafu,” amsema Bw. Mselemu.

Amneongeza katika kuongeza jitahada za halmashauri za kutunza mazingira kwa kupanda miti kwa mwaka wa fedha 2023/24 tayari wamepanda miti milioni 1.7 na kuvuka lengo la serikali la kupanda miti milioni 1.5.

Kaulimbiu ya Mbio za Mwenge Kitaifa 2024 inasema “Tunza Mazingira na Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Ujenzi wa Taifa Endelevu.”

Settings