Makamu wa Rais: Suala la upandaji miti ni la lazima

Mar, 27 2023

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango amesema suala la kupanda miti ni lazima na kuzitaka Halmashauri zote nchini kusimamia kwa karibu na kuhakikisha kwamba mazingira ya maeneo yao yanakuwa ya kijani, safi na ya kuvutia na zoezi hilo liwe endelevu.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa akizundua kampeni ya kupanda miti kitaifa kwa hisani ya Benki ya NMB ikishirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), uzinduzi uliofanyika katika eneo la Mtumba Jijini Dodoma leo tarehe 27 Machi 2023. Amesema Wakurugenzi wa Halmashauri zotenchini wanapaswa kutoa maelekezo kwa shule, taasisi mbalimbali na kwa wananchi ili washiriki kikamilifu katika uhifadhi na usafi wa mazingira.

Vilevile Makamu wa Rais ameziagiza Halmashauri kwa kushirikiana na TFS, kupanda aina za miti ambayo inaendana na mazingira ya maeneo waliopo pamoja na kuiwezesha jamii hususani ya vijana kupata elimu zaidi kuhusu utunzaji wa miti ili kuhakikisha wanachangia katika uhifadhi wa mazingira kwa weledi.

Halikadhalika Makamu wa Rais amesema Serikali inafahamu na kuthamini mchango mkubwa unaotolewa na sekta binafsi pamoja na taasisi za kidini hapa nchini katika kuhakikisha utekelezaji wa mipango mbalimbali ya uhifadhi wa mazingira inakuwa na mafanikio. Pia ametoa wito kwa taasisi hizo kuongeza juhudi hasa katika kuhamasisha, kukuza uelewa na kujenga uwezo wa jamii na taasisi mbalimbali kuhusu hifadhi ya mazingira pamoja na kutafuta rasilimali fedha zitakazo changia utekelezaji wa Sera ya Mazingira. Ametoa rai kwa Benki ya NMB kuona uwezekano wa kutumia umoja wa Mabenki (TBA) kuongeza nguvu zaidi katika kuifanya Dodoma kuwa ya kijani kwa muda mfupi zaidi kwa kutambua ndio makao makuu ya nchi.

Kwa Upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt. Selemani Jafo amesema ajenda ya upandaji miti nchini ni maelekezo ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi inayotaja kupanda miti milioni 1.5 kwa kila halmashauri na miti milioni 40 kwa mkoa wa Dodoma pekee katika kipindi cha miaka mitano. Dkt. Jafo ameipongeza Benki ya NMB kwa jitihada wanazozifanya katika kushirikiana na serikali kwenye uhifadhi wa mazingira.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB Ruth Zaipuna amesema Benki hiyo itapanda miti milioni 1 kwa mwaka 2023 nchi nzima na kuitunza kuhakikisha inafikia lengo. Ameongeza kwamba Benki hiyo itaendesha shindano maalum la upandaji miti mashuleni litakalofahamika kama “kuza mti tukutuze” ambapo kupitia shindano hilo litakalofanyika kwa mwaka mmoja na nusu shule zitashindana kutunza miti watakayokabidhiwa na TFS.

Amesema pamoja na zawadi mbalimbali zitakazotolewa lakini pia shule itakayoweza kupanda miti 2000 na kukuza asilimia 80 na zaidi ya miti hiyo itafanikiwa kupata zawadi ya shilingi milioni 50. Bi Zaipuna amesema Benki ya NMB inatambua wajibu ilionayo katika jamii kuhakikisha wanatunza mazingira ili utendaji wa kazi kuwa mzuri na bora zaidi kwani mazingira yanapoharibika hakuna kundi linalobaki salama.

Kamishna wa Uhifadhi Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania Prof. Dos Santos Silayo amesema TFS itashirikiana vema na NMB kuhakikisha wanatekeleza vema adhma ya upandaji miti milioni 1 kwa kutoa miongozo mbalimbali ya kitaalamu na kushirikiana nao katika kila Nyanja kuhakikisha adhma hiyo inafanikiwa.

Aidha Prof. Silayo amesema ushirikiano baina ya NMB na TFS utasaidia katika kuongeza wigo wa upatikanaji wa miche ya miti jamii mbalimbali katika maeneo mbalimbali nchini na kuipanda kwa weledi kuhakikisha inastawi. Ametoa wito kwa wadau mbalimbali kuendelea kujitokeza kusaidiana na serikali katika kuongeza nguvu kwenye uhifadhi katika kutekeleza kazi mbalimbali zinazopunguza utegemezi wa misitu na hasa kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa misitu, upandaji miti na kuhifadhi mazingira.

Katika uzinduzi wa kampeni hiyo zaidi ya miti 3000 imepandwa katika eneo la Mtumba jijini Dodoma.

Settings