Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa rai kwa nchi wanachama wa Mkataba wa Usimamizi endelevu wa Ziwa Tanganyika kuhakikisha wanasimamia kikamifu rasilimali zilizopo katika Ziwa Tanganyika kwa mustakabali wa maendeleo endelevu.
Akifungua Mkutano wa tisa wa Mawaziri wa nchi Wanachama wa Mkataba wa Usimamizi endelevu wa Ziwa Tanganyika leo tarehe 16 disemba, 2021 Mkoani, Makamu wa Rais amesema ni vema sasa kuunganisha nguvu kwa pamoja kuwa na msimamo wa pamoja kama nchi wanachama ili malengo na maazimio ya pamoja yaweza kufkiwa.
Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Hamad Chande amesema Tangu kupitishwa kwa Mkataba wa Usimamizi Endelevu wa Ziwa Tanganyika wamefanikiwa kuandaa na kutekeleza kwa pamoja Mpango wa Maendeleo wa Kanda ya Ziwa Tanganyika (PRODAD) ambao ulikuwa na miradi mikubwa mitatu.
“Uwepo wenu hapa Mawaziri wa Mazingira wa Burundi, Congo na Zambia unadhihirisha umuhimu wa Mkutano huu na dhamira yenu katika utekelezaji wa Mkataba wa Usimamizi Endelevu wa Ziwa Tanganyika Chande alisisitiza.
Aidha, tangu kupitishwa kwa Mkataba wa Usimamizi Endelevu wa Ziwa Tanganyika Mamlaka ya Ziwa Tanganyika imefanikiwa kukuza mipango ya maendeleo endelevu ikijumuisha uboreshaji wa miundombinu ya kimsingi, ufadhili wa maendeleo ya ndani na usimamizi shirikishi kupitia miradi tofauti
Tanzania ikiwa ni miongoni mwa nchi wanachama imeendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli zote zinazolenga kuhakikisha usimamizi endelevu wa Rasilimali za ziwa Tanganyika ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa programu za kikanda zinazolenga kulinda rasilimali za maji na Ziwa Tanganyika.
Akitoa neno la Ukaribisho, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Bi. Mary Maganga amesema Mamlaka ya Usimamizi endelevu wa Ziwa Tanganyika inaundwa na mataifa yenye mila na tamaduni mbalimbali wenye lengo moja la Uhifadhi na Usimamizi endelevu wa Ziwa Tanganyika na Bonde lake.