Makamu wa Rais awataka viongozi kudhibiti uharibifu wa mazingira

Nov, 09 2022

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango amewataka wakuu wa mikoa, viongozi wa wilaya na bodi za mabonde ya maji kufanya jitihada za ziada katika udhibiti wa uharibifu wa mazingira unaotokana na shughuli za kibinadamu ili kukabiliana na uharibifu na upoteaji wa vyanzo vya maji nchini.

Makamu wa Rais amesema hayo leo tarehe 09 Novemba 2022 alipotembelea mitambo ya uzalishaji Maji ya Ruvu Chini iliopo mkoani Pwani na kupokea taarifa ya hali ya uzalishaji na upatikanaji wa maji katika Mikoa ya Dar es salaam na Pwani. Amezitaka Wizara za Mifugo, Kilimo, Maji, Ardhi, Maliasili na Utalii , Muungano na Mazingira pamoja na sekta zote husika kushirikiana kwa karibu katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za uharibifu wa mazingira na kupata suluhu ya pamoja kwa manufaa ya taifa lote la Tanzania.

Makamu wa Rais ameitaka Wizara ya Maji kwa kushirikiana na Tamisemi kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya uchimbaji wa visima na mabwawa ili kupunguza adha ya upatikanaji wa maji inayojitokeza hivi sasa. Pia ameiagiza Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) kuhakikisha mgao wa maji unafanyika kwa haki bila upendeleo wa maeneo katika kipindi hiki cha kukabiliana na upungufu wa maji Kotoka vyanzo mbalimbali vya uzalishaji.

Makamu wa Rais amekemea vikali tabia ya wananchi kuandaa mashamba na malisho mapya kwa kuchoma moto na kueleza kwamba tabia hiyo imekua ikichangia kwa kiasi kikubwa uteketezaji wa misitu mbalimbali nchini. Aidha amewaasa wananchi hususani wakulima na wafugaji kuacha kujichukulia hatua mkononi wakati wa migogoro inapotokea. Makamu wa Rais ameviagiza vyombo vya dola kutenda haki wakati wote kwa wale wanaofanya jinai ikiwemo kuingiza mifugo katika mashamba ya mazao.

Halikadhalika Makamu wa Rais ameitaka wizara ya Mifugo na Uvuvi kuweka malengo ya kufanya sensa ya mifugo kwa lengo la kupata idadi pamoja na maeneo iliopo hatua itakayosaidia kupunguza mifugo na ufugaji wa kuhamahama.

Pia Makamu wa Rais ameziagiza Wizara za Madini na Nishati kuongeza kasi ya uzalishaji wa Nishati ya mkaa Mbadala wa kupikia ili kuondokana na mkaa unaotokana na ukataji miti unaochangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira.

Vilevile Makamu wa Rais ameitaka Wizara ya Kilimo kufanya utafiti wa kina kwa kuanza na mabonde ya kimkakati na kubaini njia zinazotumika kusafirisha maji na kiasi cha maji kinachorudi katika mto husika. Pia amewaagiza viongozi wa wizara ya kilimo kuwasimamia wakandarasi wanaotekeleza miradi ya uchimbaji mabwawa kufanya hivyo kwa kasi ya ziada ili kuharikisha kilimo cha umwagiliaji.

Kwa upande wake Waziri wa Maji Jumaa Aweso amesema Wizara itaendelea kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama na kuondokana na changamoto za upatikanaji wa maji zilizojitokeza. Aweso amesema tayari ushirikiano unafanyika na taasisi na watu binafsi wenye visima vikubwa ili waweze kuhudumia wananchi wanaokabiliwa na adha ya maji katika jiji la Dar es salaam. Ameongeza kwamba tayari jumla ya visima 160 vimefufuliwa mkoani Dar es salaam na vinazalisha zaidi ya lita milioni 26.

Katika hatua nyingine Waziri Aweso amesema serikali imepata mkandarasi wa kujenga mradi wa Bwawa la Maji la Kidunda la mkoani Morogoro ambao unatarajiwa kusaidia katika kilimo cha umwagiliaji, uzalishaji umeme pamoja na upatikanaji wa maji ya uhakika.

Viongozi mbalimbali wa Wizara walioambatana na Makamu wa Rais katika ziara hiyo wameeleza mipango ya kukabiliana na uharibifu wa mazingira katika sekta za kilimo, mifugo pamoja na maliasili na utalii.

Settings