Makamu wa Rais awapa maelekezo Mawaziri, Makatibu Wakuu

May, 18 2024

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango leo tarehe 18 Mei 2024 amefungua Warsha ya Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu kuhusu utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai iliyofanyika Ukumbi wa Kambarage mkoani Dodoma.

Akifungua Warsha hiyo, Makamu wa Rais amesema Azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuwepo kwa mfumo imara, wenye kuzingatia haki na misingi ya utawala bora katika kuwahudumia wananchi. Ameongeza kwamba nia ya dhati ya Rais ni kuleta mapinduzi ya kifikra na mabadiliko ya kimfumo katika utendaji wa taasisi za Haki Jinai hapa nchini.

Makamu wa Rais amewataka Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu kutekeleza ipasavyo mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai kwa kuwa Wananchi wameonesha hitaji la mabadiliko katika utendaji wa taasisi za haki jinai ili kuongeza uwezo na kuhakikisha haki inatendeka. Amewasihi kufahamu kwa kina msingi wa mapendekezo hayo na kujipanga kikamilifu kuyatekeleza.

Pia amewaasa viongozi hao kuendelea kuwasimamia na kuwakumbusha watumishi walio katika Wizara na Taasisi wanazosiamamia kuzingatia maadili, weledi na nidhamu katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuwaletea wananchi maendeleo.

Makamu wa Rais amesema Serikali inafanya jitihada na kutumia rasilimali nyingi katika kuboresha huduma za jamii, ikiwa ni pamoja na kusogeza huduma karibu na Wananchi kwa kuanzisha maeneo mapya ya kiutawala hivyo ameagiza TAMISEMI, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na Wizara ya Ujenzi kushirikiana ili kusimamia uanzishwaji wa ofisi za vyombo vya utoaji haki katika maeneo hayo.

Halikadhalika Makamu wa Rais amesema Utawala bora katika utumishi wa umma ni dhana inayohusisha usimamizi na utekelezaji wa shughuli za kila siku kwa kuzingatia misingi ya sheria, haki, usawa, uwazi na uwajibikaji.

Settings