Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema suala la kuhakikisha jamii inaishi katika maadili mema linahitaji ushirikiano wa pamoja wa serikali na wananchi wote.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akiwahutubia wananchi wa Wilaya ya Tabora katika Mkutano wa hadhara uliyofanyika katika Uwanja wa Chipukizi Manispaa ya Tabora. Amewasihi viongozi wa dini kuhakikisha walimu wa dini wanapatikana mashuleni na kufundisha maadili mema ili kubaliana na vitendo viovu ikiwemo mauaji pamoja na ukatili kwa watoto.
Amehimiza viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa mila, viongozi wa serikali, wazazi na walezi kuongeza jitihada katika kufundisha maadili maadili mema kwa jamii.
Makamu wa Rais amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Tabora Paul Chacha na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa huo kwa kufanikisha kuwakamata wahusika wa utekaji na mauaji katika mkoa huo. Amewataka kuendelea kuongeza juhudi kudhibiti uhalifu na kuwafikisha katika vyombo vya sheria wahusika wote.
Aidha Makamu wa Rais amekemea vitendo vya uharibifu wa miundombinu ya barabara mkoani Tabora ambapo ameagiza kuanzia ngazi ya viongozi wa serikali za mitaa kuwakamata wahusika na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.
Pia ametoa wito kwa madereva na watumiaji wa barabara kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kukabiliana na ajali za barabarani zinazogharimu maisha ya watu. Ametoa rai kwa askari wa usalama barabarani katika mikoa yote nchini kuendelea kufanya kazi za doria na kuwachukulia hatua wote wanaokiuka sheria za barabarani.
Makamu wa Rais amewahimiza wananchi wa mkoa wa Tabora kulinda na kuhifadhi mazingira ili kuepukana na mabadiliko ya tabianchi. Ametoa msisitizo wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wananchi hao ili kuokoa mazingira na kulinda afya zao.
Halikadhalika Makamu wa Rais amemuagiza Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe kuangalia namna makampuni ya ununuzi wa tumbaku yatakavyoweza kuwasaidia wakulima wa zao hilo nishati safi ya kupikia pamoja na kushiriki katika kugharamia namna bora ya kukausha tumbaku.
Makamu wa Rais amewataka Viongozi na Watumishi wa umma kuacha tabia za kukaa ofisi pekee bali wawatembelee wananchi katika maeneo yao ili kufahamu zaidi changamoto zinazowakabili.
Awali Makamu wa Rais ameweka Jiwe la Msingi Mradi wa Ujenzi wa Jengo la Abiria katika Uwanja wa Ndege Tabora pamoja na ukarabati wa uwanja huo unaogharimu shilingi bilioni 24.6.