Makamu wa Rais ahimiza usimamizi wa mazingira kukabili ukame

Jun, 05 2024

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema ili kufanikisha juhudi za kuhuisha ardhi iliyoharibiwa, kujenga ustahimilivu dhidi ya ukame na kuzuia kuenea kwa jangwa ni muhimu Taifa liimarishe menejimenti na usimamizi wa mazingira ikiwemo kupima na kuzingatia matumizi bora ya ardhi pamoja na kubadili mfumo wa ufugaji.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete Mkoani Dodoma. Amesema inahitajika wafugaji kuanza kufuga kisasa kwenye mashamba yao ya mifugo na kudhibiti idadi kubwa ya mifugo inayozidi uwezo wa upatikanaji wa malisho. Pia amesisitiza umuhimu wa kubadili kilimo ili kiwe endelevu na cha kisasa zaidi, kinachozingatia matumizi ya mboji na marejea, matumizi ya matandazo ya majani ili kuhifadhi unyevu, matumizi ya teknolojia za kijani pamoja na kudhibiti uchomaji hovyo wa misitu na vichaka.

Halikadhalika Makamu wa Rais ameziagaiza Halmashauri zote nchini kusimamia ipasavyo utekelezaji wa sheria ndogo za kulinda mazingira na kuhakikisha hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi ya wanaokwenda kinyume na sheria hizo. Amewasihi viongozi wa Serikali, Bunge, Chama, Dini na Asasi za kiraia kuungana katika kupaza sauti ili kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira.

Aidha Makamu wa Rais ametoa rai kwa Halmashauri zote kufanya jitihada kuhamasisha na kuvutia viwanda vyenye teknolojia ya kubadili taka za aina mbalimbali ili ziweze kutumika tena kama bidhaa. Pia ametoa wito kwa wananchi na sekta binafsi kuchangamkia fursa zilizopo katika ukusanyaji na urejelezaji wa taka hapa nchini.

Makamu wa Rais amesema ili kufanikiwa kupunguza na hatimaye kukomesha kabisa uharibifu wa mazingira ni lazima kutafsiri maneno kuwa vitendo katika ulinzi ,usimamizi, na utunzaji wa mazingira na kuimarisha ushirikiano wa dhati kati ya Serikali, Asasi zisizo za Kiserikali, Sekta Binafsi,Wasanii, Taasisi za Kidini, Viongozi wa Mila na wananchi kwa ujumla.

Makamu wa Rais amesema katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira, Serikali imechukua hatua mbalimbali zinazojumuisha kupitishwa kwa Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021, Mpango Kabambe wa Taifa wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (2022-2032) na kuongeza kasi ya upimaji na umilikishaji wa ardhi kimila na uhamasishaji wa matumizi endelevu ya ardhi hususan kilimo mseto, kilimo cha matuta, kilimo hifadhi na mbinu endelevu za kiasili za hifadhi ya malisho. bahari, maziwa na rasilimali nyingine za maji.

Katika Maadhimisho hayo Sera ya Taifa ya Uchumi wa Buluu ya mwaka 2024 na Mkakati wa Utekelezaji wa Sera hiyo kwa kipindi cha mwaka 2024 – 2034 imezinduliwa. Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni kuhuisha ardhi iliyoharibiwa, kuzuia kuenea kwa jangwa na kujenga ustahimilivu dhidi ya ukame.

Settings