Makamu wa Rais aelekeza mifumo ya kudhibiti magonjwa ya mlipuko iimarishwe

May, 09 2024

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ameilekeza Wizara ya Afya kwa kushirikiana na TAMISEMI kuziwezesha Idara za Afya katika Halmashauri za Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya ili kuimarisha mifumo na miundombinu ya kutambua, kudhibiti na kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa Maadhimisho ya Miaka 50 ya Kampeni ya Mtu ni Afya na Uzinduzi Awamu ya Pili ya Kampeni ya Mtu ni Afya yaliyofanyika Kibaha Mkoani Pwani. Amesema kuziwezesha Idara za Afya pia kutaimarisha mifumo ya ufuatiliaji na utambuzi wa magonjwa, kujenga uwezo wa utayari katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko, kujenga uwezo wa kufanya tafiti kuhusu magonjwa mbalimbali pamoja na kujenga mifumo ya usimamizi na upimaji matokeo ya kampeni hiyo.

Aidha Makamu wa Rais amesema amezitaka Halmashauri zote kuwatumia vizuri wahudumu wa afya ngazi ya jamii katika utekelezaji wa kampeni hiyo ambao pamoja na mambo mengine watawezesha kufikiwa kwa sehemu kubwa ya jamii, kuchochea mabadiliko ya tabia za wananchi na kuhakikisha usawa na urahisi katika utoaji wa huduma.

Vilevile Makamu wa Rais amewahimiza wananchi kujikinga na magonjwa kwa kufuata maelekezo na ushauri unaotolewa na wataalam wa afya katika ngazi mbalimbali ikiwemo lishe bora, mazoezi ya viungo na upimaji wa afya mara kwa mara. amewasihi kujenga desturi ya kufanya usafi ili kujiepusha na magonjwa yatokanayo na uchafu.

Makamu wa Rais ametoa wito kwa Vyombo vya Habari, Wasanii na vikundi vya burudani kutoa hamasa na kuelimisha jamii ili kuongeza uelewa na kufuata maelekezo yanayolenga kujenga afya ya jamii. Amesema vyombo vya habari vina jukumu kubwa la kuhamasisha na kuelimisha jamii kwa kupeleka ujumbe kwa njia mbalimbali za kibunifu na kuhakikisha kampeni zinazolenga kutoa elimu na hamasa zinakuwa endelevu na zenye kupimika.

Uzinduzi wa Kampeni ya Mtu ni Afya Awamu ya Pili umeenda sambamba na utoaji zawadi kwa washindi wa Usafi wa Mazingira kwa mwaka 2023 katika Makundi mbalimbali. Kampeni hiyo ina kauli mbiu isemayo Mtu ni Afya: Afya Yangu, Wajibu Wangu”.

Mwaka 1973 Serikali ilizindua rasmi kampeni ya MTU NI AFYA, iliyolenga kupambana na adui Maradhi. Kampeni hii ilitekelezwa kwa hatua na kwa namna mbalimbali kwa kipindi cha takriban miaka hamsini hadi sasa.

Settings