Kiongozi wa Mbio za Mwenge aridhishwa upandaji miti Pemba

Jun, 07 2023

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2023 Bw. Abdalla Shaibu Kaim amekipongeza Chuo cha Mafunzo Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini, Pemba kwa hatua za upandaji miti.

Bw. Kaim ametoa kauli hiyo Juni 05, 2023 wakati Mwenge wa Uhuru ulipowasili wilayani humo kwa ajili ya kukagua miradi mbalimbali ikiwemo ya wa utunzaji mazingira.

Amesema faida kubwa ya upandaji wa miti ni kusaidia kuhifadhi mazingira hivyo kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi zinazoikumba nchi yetu na dunia kwa ujumla.

“Ndugu zangu tuendelee kupanda miti ili kuhifadhi mazingira na hatua hii inaunga mkono juhudi za Serikali katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi,“ amesisitiza Bw. Kaim.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Wete Mhe. Hamad Omar Bakari ameahidi kuendelea kusimamia zoezi la upandaji miti katka maeneo mbalimbali nchini humo.

Amesema kuwa zoezi la upandaji wa miti katika eneo hilo unaakisi kaulimbiu ya mbio hizo kwa mwaka huu inayohimiza usimamia wa mazingira hasa kwenye vyanzo vya maji.

Aidha, Mkuu wa Wilaya amewataka wananchi kuacha kukata miti ovyo kwani hali hiyo inaweza kusababisha uharibifu wa mazingira.

Akisoma risala mbele ya kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge 2023, Kamanda wa Chuo hicho cha Mafunzo Abrahman Mwinyi Chumu alisema wameamua kupanda miti ili kurejeshea mazingira kutokana na uharibifu uliofanyika.

Aliongeza kuwa jumla ya ekari 792 zimetengwa kwa ajili ya shughuli mbalimbali zikiwemo upandaji miti ambapo wanatarajia kupanda miti aina ya mivinje 1,500 na kufanya idadi ya miti yote itakayopandwa kufikia 9,000.

Mwenge wa Uhuru unaendelea kukimbizwa katika mikoa mbalimbali nchini na kwa mwaka 2023 unachagizwa na kaulimbiu isemayo “Tunza Mazingira, Okoa vyanzo vya Maji kwa Ustawi wa Viumbe hai na Uchumi wa Taifa”.

Hivyo, katika mbio hizo zoezi la utoaji wa elimu kuhusu umuhimu wa hifadhi ya mazingira inayoendelea kutolewa kwa wananchi wanaojitokeza katika maeneo mbalimbali unakopita.

Settings